MBUNGE wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya masuala ya Ukimwi, Afya ya Mama na Watoto ya Taasisi ya Mabunge Duniani (IPU). Dk Ndugulile amechaguliwa katika mkutano wa 134 wa Mabunge duniani unaoendelea mjini Lusaka, Zambia.
Mkutano huo ulioanza Machi 17, mwaka huu unatarajia kuisha keshokutwa. Kabla ya kuchaguliwa kwake, Dk Ndugulile alikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Kamati hiyo inajumuisha wabunge wasiozidi 12 ambao huteuliwa na Rais wa IPU kutokana na umahiri na mchango wao katika masuala ya Ukimwi na masuala ya afya ya mama na watoto.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo wanatoka nchi za Armenia, India, Bangladesh, Afrika Kusini, Rwanda, Italia, Ubelgiji, Austria, Sweden, Dominica na Marekani.
Majukumu ya Kamati hiyo ni kushauri, kujengea uwezo na kuhamasisha mabunge duniani kuhusiana na njia bora za kuboresha huduma za Ukimwi pamoja na afya za akinamama na watoto.
Dk Ndugulile ni daktari bingwa katika magonjwa ya maambukizi na pia kwenye afya ya jamii. Pamoja na majukumu hayo mapya, pia mbunge huyo ni Mwakilishi wa bara la Afrika katika Taasisi ya Kimataifa ya Ukimwi, Mjumbe wa Kamati ya Wabunge Duniani kuhusu masuala ya Kifua Kikuu (TB) na Mwakilishi wa Bunge la Tanzania kwenye Bunge la Afrika.
Post a Comment