Picha ya maktaba
Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro, wilayani Kilombero jana lilimkamata mbunge wa jimbo la Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali kwa madai ya kutaka kuingia katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kuapisha na kuchagua mwenyekiti na makamu wake wakati si mpigakura.
Lijualikali alikamatwa nje ya ukumbi wa halmashauri na polisi na kuswekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Kilombero saa 3.48 asubuhi wakati akiingia kwenye ukumbi huo kama mmoja wa mashuhuda.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kilombero, Shabaan Mikongolo alisema mbunge huyo hakutendewa haki na polisi kwa kuwa alifika eneo hilo kushuhudia matukio ya kuapishwa kwa madiwani.
“Ni kama kuna maelekezo yalitolewa kwa polisi kuwazuia wabunge, Lijualikali na Devotha Minja (Viti Maalumu – Chadema) na mwakilishi wa Katibu Mkuu Chadema kutoingia ukumbini lakini viongozi wengine wa Serikali ngazi ya mkoa na wilaya waliruhusiwa." Alisema Mikongolo
Pia, polisi walizuia waandishi wa habari na kutaka kuwanyang’anya kamera zao kwa sababu ambazo hazikuwekwa bayana.
Katika uchaguzi huo, Diwani wa Sanje (CCM), David Ligazo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilombero kwa kura 19 dhidi ya Godfrey Lwena ( CHADEMA) aliyepata kura 18
Post a Comment