Katika jitihada za kuongeza makusanyo ya mapato ya serikalii, Mamlaka ya Mapato (TRA), imejiwekea lengo la kukusanya Sh. trilioni 1.3 kwa mwezi Machi.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi wa Mamlaka hiyo, Diana Masalla, wakati akizugumza na Nipashe kuhusu malengo ya mwezi huu.
“Kwa mwezi wa Machi lengo ni kukusanya Sh.trilioni 1.3, kiasi hiki ni lengo lakini tunaweza kuvuka na kufikia zaidia ya hapo,” alisema Massala.
Tangu serikali ya Rais John Magufuli iingie madarakani Novemba 5, mwaka jana, ukusanyaji wa kodi umekuwa ukiongezeka na kushuka.
Kwa mwezi Novemba mwaka jana, mapato ya TRA yalipanda kutoka wastani wa Sh. bilioni 800 kwa mwezi mpaka Sh. trilioni 1.3.
Aidha, mwezi Desemba mwaka jana ukusanyaji huo uliongezeka hadi kufikia rekodi ya Sh. trilioni 1.4, lakini Januari makusanyo yalikuwa Sh. trilioni 1.06.
Kiasi hicho kilikwenda chini mwezi uliopita ambapo TRA ilikusanya Sh. trilioni 1.04.
Itakumbukwa kuwa wakati akilihutubia Bunge mjini Dododoma Novemba 20, mwaka jana, Rais Dk. Magufuli alisema Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ukusanyaji wa mapato umekuwa chini kwa sababu mbalimbali.
Alisema Serikali ya awamu ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
“Tutahakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki. Hatutasita kumchukulia hatua mtu yoyote atakaye kwepa kulipa kodi," alisema Rais Magufuli.
"Tunawaomba wananchi mhakikishe mnapewa risiti kila mnaponunua bidhaa au huduma maana kodi ni kitu muhimu lazima kila mtu anayestahili kulipa kodi alipe.”
Rais Magufuli pia alieza kuwa serikali yake itahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi kwa kuziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi.
Loading...
Post a Comment