WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepewa jina jipya la Kisukuma na kukabidhiwa zana nyingine muhimu katika vita ya kupambana na ufisadi nchini maarufu kwa jina la kutumbua majipu.
Kuanzia juzi, Waziri Mkuu Majaliwa atakuwa akifahamika kwa jina lingine la Masanja, alilopewa na Wazee wa Kisukuma wa Lamadi wilayani Busega katika mkoa wa Simiyu.
Kabla ya kuwahutubia maelfu ya wakazi wa Lamadi juzi jioni, wazee hao walimvisha Waziri Mkuu vazi la kijadi la Kisukuma akiwa katika kigoda, wakamkabidhi usinga, ng’ombe wawili na mkuki ambao walimueleza kuwa kazi yake ni kuendeleza vita ya ufisadi kwa kuutumia kutumbua majipu.
“Tunakukabidhi usinga na huu mkuki utumike kutumbua majipu kwa sababu kazi hii unaifanya vizuri hadi sasa, kwa hiyo uendelee kutumbua majipu. Na kwa kuanzia sasa, tunakupa jina la kwetu, kwa sababu wewe ni kijana wetu, utaitwa Masanja,” alisema Mchele Malale kwa niaba ya wazee wenzake.
Kwa mujibu wa wenyeji, jina la Masanja lina maana ya kuingia kokote, hali inayomaanisha kuwa Waziri Mkuu Majaliwa aendelee kutumbua majipu kila mahali.
Alipoanza kuhutubia, Waziri Mkuu alikiri kuwa amepata mapokezi makubwa kwa wananchi wa Lamadi, na zaidi, makubwa kuliko sehemu nyingi alizokwenda tangu ashike wadhifa wake huo.
“Kwa kweli nimefurahishwa na mapokezi yenu hapa…tangu nilipotoka Mwanza hadi kufika kwenu (Busega) mapokezi yamekuwa mazuri, na hapa Lamadi mmetisha. Mmenitia faraja sana,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza:
“Lakini nimefurahi kwa zawadi mlizonipa na pia jina jipya la Masanja.Nimeandika pale kwenye diary (shajala) yangu. Mmenipa pia mkuki, mmesema nitumie kama sindano kuendeleza ile kazi,” alisema Waziri Mkuu na kushangiliwa na maelfu ya wakazi wa Lamadi.
Akiwa Bariadi jana, Waziri Mkuu alisema jina lake sasa ni Masanja Mkusanyaji, na kwamba ataendelea kukabiliana na wakwepa kodi na mafisadi ili Watanzania wapate huduma stahiki.
Post a Comment