Waziri wa
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa amekagua mradi wa
upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco yenye kilomita 4.3 ambapo
ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 95.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara hiyo
Prof.Mbarawa ameeleza kuwa tayari njia tano zimeanza kutumika kuanzia
eneo la Mwenge hadi Kijitonyama zenye urefu wa kilomita 2 huku kilomita
nyingine 2.3 zikiwa katika harakati za mwisho za kukamilishwa.
“Serikali
imedhamiria katika kuhakikisha kuwa inatatua kero ya msongamano wa
magari kwa kufanya upanuzi wa njia muhimu ili kurahisisha hali ya
usafiri jijini Dar es Salaam ” alisema Prof.Mbarawa.
Aliongeza
kwa kusema hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli alizindua mradi wa daraja la Kigamboni
linalounganisha kurasini na Kigamboni pamoja na kuweka jiwe la msingi
kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa flyover katika eneo la Tazara .
Kwa
upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)
Mhandisi.Patrick Mfugale ameeleza kuwa mradi huo umekabiliana na
changamoto mbalimbali ikiwemo uhamishaji wa mabomba ya maji safi na maji
taka katika eneo la Makumbusho na Mwenge ili kuendelea na ujenzi.
Novemba
30 mwaka jana Rais John Magufuli aliagiza kiasi cha shilingi bilioni
nne kilichopangwa kutumika katika shamrashamra za siku ya Uhuru kitumike
katika kazi ya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es
salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 ili kuiunganisha barabara hiyo na
ile ya Mwenge – Tegeta yenye urefu wa KM 12 .
Post a Comment