CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema, Rais John Magufuli ni mkwapuaji,anaandika Dani Tibason.
Kimeeleza, Rais Magufuli amekwapua sera za chama hicho kwa pupa lakini hana uwezo wa kuzitekeleza kwa kiwango kinachokubalika.
Pia kimeeleza, Rais Magufuli anatokana na chama chenye misingi ya wizi-Chama Cha Mapinduzi (CCM)-na kwamba, serikali yake haiwezi kuwa na safi.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Dk. Vicent Mashinji, Katibu wa Mkuu wa chama hicho-Taifa wakati akifungua kongamano la Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) na Umoja wa Wanachadema Vyuo Vikuu (CHASO).
Katika hotuba yake Dk. Mashinji amedai kuwa, Rais Magufuli amekuwa akifanya maigizo ya utumbuaji majipu kwa baadhi ya watumishi ili kuwaaminisha Watanzania kwamba, kazi anayoifanya ni sahihi.
Hata hivyo amesema, Chadema hawapingi utumbuaji wa majipu na kwamba, ni lazima utumbuaji huo ufuate sheria na kanuni za utumishi wa umma.
“Nawakumbusha masuala ya haki, hakuna haki bila wajibu. Watawala wanatuongelea sisi, mbona wao hawajiongelei, kwetu sisi wajibu wao ni kufuata kanuni za nchi. Hivi hawa mawaziri wamefanya kazi gani mpaka sasa,’’amehoji Dk. Mashinji.
Dk. Mashinji amesema, kwa sasa tatizo kubwa lililopo nchini ni mfumo uliowekwa na viongozi waliopita ambao wengi walikuwa wala rushwa.
“Tatizo la rushwa ni mfumo, ukiona mmoja katajwa ujue kuna 100 wapo nyuma yake. Hata hili la kuazishwa Mahakama ya Mafisadi limewahi kufanywa mwaka 1983 lakini halijasaidia,’’ amesema.
Katibu huyo amewataka vijana kuacha woga ili kuwa na Taifa makini katika miaka ya baadaye, “vijana kuweni makini, kumbukeni Taifa linawategemea.”
Hata hivyo, Dk. Mashinji amepinga vikali hatua ya serikali kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya bunge kwa kuwa, vinanyima wananchi haki ya kupata habari.
‘Bunge ni kama mkutano wa hadhara, kila mtu anatakiwa aone kila kitu. Ukiona mtu anaficha kitu ujue kuna jambo, hapa kuna walakini lazima vijana mpige kelele,’’ amesema.
Pia amewataka vijana hao kutumia elimu kulikwamua Taifa, “sisi Chadema tunatoka katika elimu ya msingi na tunaenda katika elimumsingi, naombeni msome ili muokoe Taifa hili kwani linakufa,’’ amesema.
Kwenye mkutano huo Julius Mwita, Katibu wa Bavicha amewataka vijana kuhakikisha wanasimama kidete katika kusaidia Chadema ili kiweze kushika dola mwaka 2020.
John Heche, Mwenyekiti Mstaafu wa BAVICHA amemshambulia Rais Magufuli kutokana na kumtumbua Wilson Kabwe, aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kwenye mkutano wa hadhara.
Heche amesema, Rais Magufuli mpaka sasa hana ujasiri wa kuwatumbua viongozi wa Wizara ya Ujenzi hususan Wakala wa Barabara nchini (TANRODS) ambao wamejenga barabara nyingi chini ya kiwango wakati akiwa waziri wa wizara hiyo.
“Sisi hatumtetei Kabwe kwani Chadema ilikuwa ya kwanza kumpigia kelele kutokana na ufisadi alioufanya.
“Lakini stahili ambayo anaitumia Magufuli ni mbaya zaidi, wanasiasa wangapi ambao wapo katika baraza lake la mawaziri ni mafisadi wa kutupwa, ni kwanini hajaweza kuwatumbua?” amehoji.
Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini amewashambulia baadhi ya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini kwa madai kuwa, ni wanafiki.
Amesema, hakubaliani na makongamano ambayo yanaandaliwa na Prof. Issa Shivji, Prof Benson Bana pia Prof. Kitila Mkumbo kwa madai, watu hao wamejaa unafiki.
Msigwa ametoa kauli hiyo wakati akiwasilisha mada katika kongamano la vijana iliyohusu Utawala wa Sheria katika awamu ya tano.
Amesema, kwa sasa nchi imejaa viongozi waoga, wanafiki, wanaojipendekeza na kuwa, wote hao wamezalishwa na utawala dhalimu wa CCM.
Katika kongamano hilo Msigwa amesema, vijana hususani wasomi ni wajibu wao kuachana na tabia ya kulalamika au kuwajengea chuki viongozi na badala yake wanatakiwa kuvaa ujasiri wa kuhoji na kutaka kupata majibu.
MwanaHalisiOnline
Loading...
Post a Comment