CHINA
imekubali kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa mradi wa
ujenzi wa reli ya kati yenye urefu wa kilometa 2,561 kwa kiwango cha
kisasa yaani "Standard Gauge" ambao zabuni za ujenzi zinatarajiwa
kutangazwa hivi karibuni.
Balozi
wa China hapa nchini Mheshimiwa Dkt. Lu Youqing ametoa kauli hiyo leo
tarehe 25 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam alipokutana na kufanya
mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli ambapo pia amemkabidhi barua yenye ujumbe kutoka kwa Rais wa
China Mheshimiwa Xi Jinping.
Katika
Mazungumzo hayo Rais Magufuli amemweleza Balozi Lu kuwa Tanzania
imedhamiria kuanza ujenzi wa Reli ya kati haraka iwezekanavyo na tayari
imetenga fedha kiasi cha shilingi Trilioni 1 katika bajeti yake ijayo
kwa ajili ya kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi huo.
"Tuna
imani kuwa mradi huu utasaidia kuleta mapinduzi makubwa ya uchumi
katika nchi yetu na katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na kati
zikiwemo Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ndio maana
hatutaki kupoteza muda kwa mazungumzo marefu, tunataka kazi ianze na
watu waanze kunufaika" Amesisitiza Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Balozi China hapa nchini Dkt. Lu Youqing amempongeza Rais
Magufuli na serikali yake kwa kujiandaa kwa fedha, vifaa na rasilimali
watu kwa ajili ya kutekeleza mradi huu mkubwa na kwamba Serikali ya
China, Taasisi za fedha za China na Makampuni mbalimbali yatatoa
ushirikiano wote katika utekelezaji wa mradi huu.
"Kama
ambavyo Prof. Mbarawa amefanya mazungumzo na Serikali ya China, Taasisi
za fedha za China na Makampuni, naahidi kuwa tutaanza kazi kama ambavyo
taratibu na viwango vya ujenzi vimewekwa, tutafanya kazi kwa kujali
muda, ubora na gharama nafuu" Amesema Balozi Lu.
Mradi
mzima wa ujenzi wa reli ya kati unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni
6.8 na umepangwa kutekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza itahusisha
ujenzi wa kilometa 1,216 za kutoka Dar es salaam - Tabora - Isaka -
Mwanza na itajengwa kwa ushirikiano wa Tanzania na China.
Tayari
Rais Magufuli amemtuma Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof.
Makame Mbarawa Mnyaa kwenda nchini China kukamilisha mazungumzo juu ya
utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa ujenzi wa reli ya kati,
ambapo Prof. Mbarawa anasema hatua inayofuata sasa ni kutangaza zabuni
ya ujenzi wa reli hiyo kwa uwazi, ili makampuni mbalimbali ya ujenzi
yaombe na hatimaye kupata washindi watakaoanza kazi mara moja.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam-25 Aprili, 2016.
Post a Comment