WAZIRI wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alisema serikali imeweka utaratibu mzuri wa fedha za ahadi ya Rais ya milioni 50 kila kijiji, ili Watanzania wote wanufaike bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Alisema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilango(Chadema) aliyetaka kusikia kauli ya serikali juu ya mgawanyo wa fedha hizo akisema ipo mizengwe kwamba fedha hizo zitatolewa kwa wanachama wa CCM .
“Serikali itoe kauli fedha hizo zitatolewa kwa utaratibu gani,” alihoji.
Mhagama alisema fedha hizo ni ahadi ya Rais aliyotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ambao Watanzania walichagua Serikali ya CCM.
Alisema serikali inatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
Alisema Baraza la Uwezeshaji Kiuchumi limeanza kutengeneza utaratibu wa namna ambavyo fedha hizo zitanufaisha Watanzania wote.
Alisisitiza kuwa serikali iko imara kuhakikisha fedha hizo zinanufaisha Watanzania wote.
Awali, Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Bulembo (CCM), katika swali la msingi, alitaka kufahamu ni lini ahadi hiyo ya kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji itatekelezwa.
Alitaka kufahamu pia vijana watapata mgao wao kwa asilimia ngapi.
Mbunge huyo pia alitaka kujua mikakati ya serikali katika kuwawezesha vijana wawe wajasiriamali kwa kuwapa mitaji, mikopo na vigezo gani vitakavyosimamia na kuwalinda na kuweka usawa wa upatikanaji wa ushiriki wao katika fursa hizo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Antony Mavunde alisema ahadi ya Rais ya Sh milioni 50 kwa kila kijiji itaanza kutekelezwa kwa mwaka wa fedha ujao 2016/2017.
Alisema utaratibu wa kugawa fedha hizo unaandaliwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Post a Comment