Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta) limepinga mpango wa Rais John Magufuli wa kukata malipo ya mishahara ya watumishi wa umma kutoka Sh40 milioni kwa mwezi hadi Sh15 milioni.
Akizungumza na viongozi wa vyama vya wafanyakazi Kanda ya Ziwa jijini Mwanza jana, Naibu Katibu Mkuu wa Tucta, Hezron Kaaya alisema uamuzi huo ni kinyume na sheria na utaligharimu Taifa iwapo wahusika wataamua kwenda mahakamani kupinga mishahara yao kupunguzwa.
“Watendaji hawa hawakujipangia mishahara wao wenyewe, bali malipo haya yalipangwa na bodi za mashirika na taasisi husika ambazo kisheria zimepewa mamlaka hayo. Malipo haya hayawezi kupunguzwa kwa kauli za kisiasa bila kuzingatia mahitaji ya kisheria,” alisema.
“Iwapo Serikali itatekeleza lengo hili bila kuwapo mjadala mpana na makubaliano ya kisheria kati ya wahusika, basi ijiandae kulipa mamilioni ya fedha kama fidia iwapo watakaokatwa mishahara yao watakwenda mahakamani.”
Akiwa mjini Chato wakati wa mapumziko ya wiki moja, Rais Magufuli alitangaza kupunguza mishahara ya juu kutoka Sh40 milioni hadi Sh15 milioni kwa mwezi, akisema wapo watumishi wa umma wanalipwa masilahi manono na kuishi kama wako peponi, huku wanaolipwa Sh300,000 wakiishi kama wako jehanamu.
Kaaya aliishauri Serikali kuendelea kuwalipa mishahara hiyo minono wahusika hadi mwisho wa mikataba yao, ndipo lengo la kuipunguza litekelezwe ama kwa kuwapa wahusika mikataba mipya au kuajiri watu wengine.
“Serikali inaweza kuwa na nia njema kupunguza tofauti kubwa ya mishahara kati ya kada ya juu na chini, lakini utekelezaji wake lazima usubiri muda mwafaka mikataba ya sasa itakapomalizika,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine; Tucta imepinga hatua zinazochukuliwa na baadhi ya mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya ya kutangaza kuwasimamisha kazi watumishi wa umma ambao hawapo chini ya mamlaka zao kinidhamu.
Post a Comment