Yassin Khalid Salum.
MWANAUME anayefahamika kwa jina la Yassin Khalid Salum, 34, mkazi wa Mtoni Mtongani jijini Dar anapitia kipindi kigumu cha mateso kutokana na tatizo linalomkabili la kutolewa mfupa kwenye fuvu lake na kuwekwa tumboni ili kuoteshwa sehemu zilizopata hitilafu, ambapo kidonda cha tumboni katika sehemu ulipowekwa mfupa huo kinamsumbua ikiwa ni pamoja na kutoa usaha mara kwa mara.
Akizungumza na gazeti hili kwa majonzi, Yassin anayejishu-ghulisha na ufundi redio na televisheni anasema alipata ajali usiku wa kuamkia Mwaka Mpya wa 2013 wakati akirejea nyumbani kwake baada ya kumaliza shughuli zake za ufundi.
Akisimulia mkasa huo, Yassin alikuwa na haya ya kusema: “Nilikuwa katika baiskeli yangu Mtongani Dar, Mtaa wa Namba Tano napandisha kilima ghafla lilitokea nyuma yangu gari lililokuwa limekatika breki na kuigonga baiskeli yangu, mimi nilikwenda kupigiza kichwa kwenye mtaro na baada ya hapo nikapoteza fahamu.
“Nilipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, baada ya kupigwa x-ray madaktari walibaini kuwa nilipata tatizo kwenye fuvu langu, ikabidi watoe sehemu ya mfupa penye tatizo wakaiweka tumboni ili kuiotesha lakini kiukweli katika sehemu hiyo ambayo wameiweka inasumbua sana.
“Mimi ni baba wa watoto watatu na kutokana na matatizo yanayonikabili, sina msaada wowote ule kwa watoto hawa malaika wa Mungu.
“Sina baba, mama yangu ni mzee hajiwezi kwa lolote lile, napata tabu maana hata kaka yangu aliyekuwa ananisaidia siku hizi hafanyi hivyo tena, naombeni msaada Watanzania wenzangu.
“Nimefuatilia kliniki kuanzia mwaka 2013 na wiki iliyopita nimeambiwa natakiwa kulazwa ili mfupa uliowekwa tumboni utolewe na kurudishwa kichwani. Huduma hiyo nimeambiwa inagharimu shilingi 200, 000 pesa ambazo nimeshindwa kuzipata hivyo naomba msaada Watanzania wenzangu,” alisema Yassin kwa huzuni.
Yeyote aliyeguswa na tatizo la mgonjwa huyo na ana nia ya kumuokoa kutoka katika mateso anayopata, awasiliane naye kwa namba ya simu 0714 972370- Mhariri.
Post a Comment