Dar es Salaam. Kauli ya Rais John Magufuli kwamba yuko tayari kuutoa mwili wake sadaka katika kupambana na rushwa na ufisadi uku kuwasaidia wanyonge, imeibua mjadala huku wanasiasa wakitofautiana.
Akizungumza katika Mkutano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema: “Unapoona watu wanashangaashangaa sana (ni) kwa sababu hawakuzoea haya. Na walifikiri nitakuwa part of them (sehemu yao), never (haitatokea), not me (si mimi).
“Ni mara 10 nisiwe rais, nikachunge hata ndege, nikakae kijijini kuliko niwe Rais halafu nivumilie uozo huu unaofanyika. I’m saying never (nasema haitatokea).”
Rais Magufuli amekuwa akizitoa kauli kama hizo mara kwa mara, hasa anapowawajibisha baadhi ya watendaji wa Serikali, huku ikidaiwa kuna upinzani mkali ndani ya chama chake cha CCM, hali inayohisiwa kusababisha kauli hiyo.
Mkurugenzi wa Fordia, Bubelwa Kaiza alisema kauli hizo za Rais Magufuli zinaonyesha uzalendo wa kweli na amefanikiwa kufanya mambo yaliyowashinda marais waliomtangulia.
“Ndani ya CCM kuna upinzani mkali kutoka kwa makada. Kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita watendaji wa Serikali wamekuwa na mikakati ya kusaidia wezi na utapeli, hivyo anachofanya ni ‘revival strategy (mkakati wa kufufua),” alisema Kaiza.
“Watendaji wa Serikali waliosimamishwa kwa kipindi kifupi cha Rais Magufuli ni wengi kuliko waliosimamishwa na Rais Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kwa pamoja. Haogopi na wala hana upendeleo,” alisema Kaiza.
Kaiza alisema tabia ya muda mrefu ya kubebana ndani ya CCM imesababisha kuwapo kwa ufisadi uliokithiri, ukiwamo uingizwaji wa dawa za kulevya na ujangili wa meno ya tembo.
Hata hivyo, msemaji mkuu wa CCM, Christopher Ole Sendeka alisema hakuna upinzani wala mpasuko ndani ya chama hicho kuhusu utendaji wa Rais.
“Sidhani kama kuna kuvutana na watu ndani ya CCM. Rais Magufuli ni mwana-CCM, kwa tafsiri yangu, amekataa kuungana na wakwepa kodi, wabadhirifu wa mali ya umma ambao baadhi yao wamo ndani ya chama na wengine wako nje,” alisema.
“Rais Magufuli anatekeleza mipango ya chama kwa asilimia 100 na hakuna mpasuko. Anachokifanya ndicho kinachotakiwa na chama.
“Unapojiunga na CCM unaapa kwamba binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja. Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote, nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma. Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa. Sasa asiyeyafuata haya ameingia kwenye chama kwa bahati mbaya.”
Alisema Magufuli hawezi kuwa kama rais wa zamani wa Malawi, Bingu wa Mutharika (marehemu) aliyejitoa chama tawala cha Democratic Progressive Party na kuanzisha Peoples Party baada ya kutoelewana na wenzake.
“Haiwezekani akajitoa CCM kwa sababu anachokifanya ndicho msingi wa CCM. Kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ ilikuwapo hata zamani, Uhuru ni Kazi, Kazi ni kipimo cha utu,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Simanjiro.
“Kwa kweli amejitoa sadaka katika taifa hili ambalo rushwa imetamalaki na kuna mafisadi wamekuwapo. Si kazi ndogo.”
Alipoulizwa kuhusu kauli hiyo, Dk Benson Bana, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema Rais Magufuli amejitoa mhanga kupambana na ufisadi, japo hataki kukitumia chama chake kwa sababu kitamharibia.
“Rais amejitoa mhanga kupambana na ufisadi, kusafisha Serikali ni ajenda yake. Tunaona yanayotokea. Yeye kama Rais alikuwa anauambia umma kwa sababu watu wanaweza kusema ni nguvu ya soda, si unajua tena watu wenye nguvu ya pesa, watafanya kila wawezalo,” alisema.
“Suala la chama kuchafuka si la leo, CCM ilishachafuka, ndiyo maana wakati wa kuomba kura, Rais Magufuli hakuwa akiitanguliza chama, na yeyote mwenye busara, huwezi kujitambulisha na CCM.
“Wilson Mkama alijitahidi akavua magamba yakakumbatiwa kwingine, akaja (katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman) Kinana na (katibu mwenezi) Nape Nnauye wakazunguka nchi nzima kujaribu kukirudisha chama kwenye mstari, lakini hiyo si kazi ya siku moja.
“Tena mimi ningekuwa mshauri, ningewashauri wamwache Rais Magufuli aongoze Serikali. Watafute mtu mwingine aongoze chama kwa sababu ukijitambulisha na CCM huwezi kuwa popular (kupendwa na wengi). Sisi tunaopita mitaani tunajua.”
Kwa upande wake, George Shumbusho kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, alisema ujumbe huo wa Rais Magufuli unatoa tahadhari kwa wafanyabiashara kuwa baadhi yao wabadilike na kuanza kutumia njia zisizokuwa na ujanja wa kukwepa kodi, vinginevyo atakuwa na uwezo wa kuwashughulikia bila kuhofia jambo lolote.
Profesa Shumbusho alisema imekuwa kawaida baadhi ya wafanyabiashara kutumia nafasi zao kushawishi viongozi wanaoingia Ikulu.
“Hata Hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema Ikulu ikiingiliwa na wafanyabiashara, Rais hawezi kukusanya kodi. Sasa labda (Rais Magufuli) ameona wanajaribu kumshawishi,” alisema profesa huyo huku akicheza.
Emmanuel Mallya, mhadhiri kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), alisema si jambo geni na baya kwa kundi la wafanyabiashara kutoa mchango wao kwa mgombea wa urais wanayempenda aingie madarakani.
Alisema duniani kote kumekuwa na makundi mbalimbali yaliyo na lengo la kushawishi mgombea fulani kuingia Ikulu, yakiamini ana uwezo wa kushughulikia masilahi yao.
“Makundi haya huitwa ‘lobby groups’. Hii si kwa nia mbaya hata waandishi huonyesha mrengo wao kushawishi ili mgombea akiingia Ikulu, awasaidie kufanikisha masilahi yao. Lakini yapo makundi ambayo hutumia nafasi hiyo kwa lengo la kupata unafuu wa kujinufaisha maslahi yao.
Hata hivyo, makamu mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema endapo Rais Magufuli ataiacha kauli hiyo bila ufafanuzi, atakuwa amewakebehi marais wastaafu waliomtangulia.
Profesa Safari alisema hakuna chama chochote cha upinzani kilichowahi kuongoza taifa hili hivyo, kauli hiyo ina maanisha wafanyabiashara ndiyo waliowaweka madarakani viongozi hao waliomtangulia.
“Kauli hiyo ni kuwabeza wenzake hao waliomtangulia kwa sababu upinzani hauhusiki na haujawahi kuongoza nchi hii. Sasa akiacha kauli hii kama ilivyo, hiyo ndiyo maana yake,” alisema.
Kwa upande wake mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema kauli hizo za Rais Magufuli hazina dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi nchini.
“Kwa ajenda ya ufisadi, Rais Magufuli kashindwa kuwawajibisha wale watu ambao hata jamii inawajua, lakini anasema anatumbua jipu hata likiwa kwenye kwapa, mbona kashindwa kuwatumbua,” alisema Mchungaji Msigwa bila ya kutaja watu ambao Rais hajawachukulia hatua.
Post a Comment