Dodoma. Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali itafanya msako katika vyuo vyote nchini ili kubaini wanafunzi waliodailiwa bila kuwa na sifa kama ilivyotokea kwa wanafunzi 480 wa Chuo Kikuu cha St Joseph.
Vilevile, amesema msako kama huo utafanyika katika maeneo ya kazi ili kubaini wafanyakazi walioajiriwa bila kuwa na sifa stahiki.
Profesa Ndalichako alisema hayo jana jioni wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge walizotoa wakati wa mjadala wa bajeti yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2016/17.
“Kazi ndiyo imeanza, haitoishia hapo (St Joseph) itakwenda na vyuo vingine. Wanaotumia vyeti wajitokeze wenyewe. Hata huko kwenye ofisi za Serikali tutafika kufanya ukaguzi,” alisema Profesa Ndalichako na kuongeza, “Inawezekana hata hapa bungeni wapo.”
Kauli hiyo ya Waziri ilitokana na michango ya wabunge waliokuwa wanahoji kuhusu hatua ya Serikali kufuta udahili wa wanafunzi wa St Joseph iliyokwenda sambamba na kuvunja Kamisheni ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.
Ada elekezi
Awali, katika mjadala, wabunge kadhaa, wakiwamo waliokuwa naibu mawaziri wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete waliitaka Serikali kuacha kuzibana shule binafsi kwa kuweka ada elekezi badala yake iboreshe mazingira ya shule zake na masilahi ya walimu ili wazazi wasione haja ya kuwapeleka watoto wao huko.
Mawaziri hao ni Philipo Mulugo aliyekuwa naibu waziri wa elimu na Daniel Nsanzungwanko aliyekuwa naibu waziri wa habari, utamaduni na michezo katika baraza la kwanza la Kikwete.
Katika mchango wake, Mulugo ambaye ni Mbunge wa Songwe (CCM), alisema wamiliki wa shule binafsi wanaendesha shule zao kwa kupata mikopo benki na pia wanalipa kodi kubwa serikalini, jambo linalowafanya kuwa katika wakati mgumu.
Aliitaka Serikali iziache shule binafsi zishindane zenyewe kwa viwango vya ada vinavyoendana na ubora wa mazingira na elimu inayotolewa.
Alisema Serikali imeweka mazingira magumu kwa walimu kutoka nje ya nchi kufundisha wakati hakuna hapa nchini walimu wanaoweza kufundisha shule zinazotumia Kiingereza.
“Mpaka sasa Tanzania haina chuo kinachofundisha walimu kwenda kufundisha kwa kutumia lugha ya Kiingereza. Serikali imeweka wigo kwa shule binafsi bila kuangalia umuhimu wa shule hizi,” alisema Mulugo ambaye pia ni mmiliki wa shule.
Mulugo aliishauri Serikali kuanzisha mamlaka huru ya udhibiti wa elimu ili kusimamia viwango na ubora wa shule zote nchini za umma na zile binafsi.
Alisema shule za umma zinaanzishwa wakati hazina viwango vya ubora vinavyotumika wakati wa kuanzisha shule binafsi. Alisema kukiwa na mamlaka huru, shule yoyote haiwezi kuanzishwa kama haijakidhi viwango vya ubora hata kama ni ya umma.
“Anayewalipa walimu ni Wizara ya Fedha; anayesimamia ubora wa elimu ni Tamisemi; anayepandisha vyeo walimu ni Utumishi; anayesimamia sera ya elimu ni Wizara ya Elimu. Kuna haja ya kuwa na chombo kimoja kitakachosimamia mambo yote haya,” alisema.
Nsanzugwanko ambaye ni Mbunge wa Kasulu (CCM), alisema kuweka ada elekezi ni kuwaonea wamiliki wa shule binafsi ambao alisema wana mchango mkubwa katika sekta ya elimu nchini.
“Serikali ikae na wamiliki wa shule binafsi ili wakubaliane namna ya kuendesha elimu. Zamani ilikuwa fahari kwa mwanafunzi kusoma shule za umma na aliyekwenda kusoma shule za binafsi alionekana amefeli. Serikali ikae na kujiuliza maswali ilikosea wapi?” alisema.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema ada elekezi hazina maana kwa sababu ya soko huria, hivyo badala ya kuishusha Serikali inatakiwa kuboresha shule zake ili ziingie kwenye ushindani na shule za binafsi.
Aliitaka Serikali kuwa na utaratibu wa kuwajengea uwezo walimu ili Taifa liwe na walimu wazuri.
Alisema bila kujenga msingi bora wa walimu, elimu bora haitapatikana hata kukiwa na mazingira bora ya kufundishia.
“Zamani wazazi walipeleka watoto wao kusoma Kenya na Uganda, hali ilikuwa mbaya hapa nchini. Leo shule hizi (binafsi) zimeanza kufanya vizuri, mnataka kuzivuruga tena? Serikali iachane na mpango huo,” alisema Lugola.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Jesca Kishoa alisema viongozi wa Serikali hawaoni uchungu wa elimu nchini kwa sababu watoto wao hawasomi shule za umma, bali kwenye shule binafsi na wengine nje ya nchi.
“Ninamuomba Rais atangaze kwamba watoto wote wa mawaziri wasome shule za Serikali. Ni aibu kuona tunajadili namna ya kuinua shule zetu wakati watoto wa viongozi wetu hawasomi katika shule hizo,” alisema.
Loading...
BLOG RAFIKI
-
-
Sh bilioni 20 zakusanywa treni ya SGR4 hours ago
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
Post a Comment