Mbunge wa Konde Khatibu Said Haji (Cuf), jana aliibua sakata la Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) bungeni akimtaja Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwamba alikiuka Katiba kwa kutoa msamaha kwa watu waliotuhumiwa.
Hata hivyo, Serikali kupitia kwa Waziri wa Katiba na Sheria Dk Harrion Mwakyembe ilikanusha madai hayo na kusema Rais alikuwa sahihi kwa kuwa viko vifungu ambavyo vinampa nafasi hiyo.
Katika swali la nyongeza, mbunge huyo alihoji ni kwa nini Kikwete alitoa msamaha kwa watu hao kabla hawajahukumiwa na Mahakama kama Katiba inavyosema.
“Kama hivyo ndivyo, basi naomba ukubali kuwa Kikwete (Rais mstaafu) alivunja Katiba ya nchi kwa kuwapa msamaha watuhumiwa wa EPA ambao walikuwa hawajahukumiwa bado, naomba majibu,” alihoji Haji.
Katika swali la msingi Mbunge huyo alitaka kujua iwapo Rais kwa mujibu wa Ibara ya 45 (1) A hadi D anayo mamlaka ya kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yake yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchunguzi/upelelezi au mahakamani.
Waziri alisema ibara hiyo ni kweli inampa mamlaka Rais ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya Mahakama kupitia kifungu cha kwanza (1).
Dk Mwakyembe alisema kifungu (ii) kinampa Rais Mamlaka ya kumwachia kabisa au kwa muda maalumu mtu yeyote aliyehukumiwa kuadhibiwa kwa kosa lolote.
“Katika kifungu cha (iii) Rais anaweza kubadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu kwa kosa lolote iwe adhabu tahafifu na kifungu cha (iv) anaweza kufuta adhabu yoyote au sehemu ya adhabu,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema kwa kuzingatia masharti ya Katiba, msamaha wa Rais unatolewa kwa mtu aliyetiwa hatiani na kupewa adhabu na Mahakama lakini watuhimiwa wa uhalifu ambao mashauri yao yako hatua za upelelezi au uendeshaji mahakamani hawaguswi na masharti ya ibara hiyo.
Alisema Rais hawezi kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo katika vyombo vya dola kwani hatima ya watuhumiwa hao inakuwa bado ipo katika mamlaka za uchunguzi, mashtaka na Mahakama.
Post a Comment