Wakati mwili wa aliyekuwa Mkuruenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe ukitarajiwa kuzikwa Jumatano ijayo kijijini wake Mamba, Mpinji wilayani Same, chanzo cha kifo chake kimetajwa kuwa ni saratani ya tezi dume na kuharibika kwa ini.
Kabwe (pichani) alifariki dunia juzi alipokuwa akitibiwa katika Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Mauti hayo yamemkuta ikiwa ni siku 38 baada ya kusimamishwa kazi hadharani na Rais John Magufuli kwa tuhuma za kuingia mikataba iliyosababisha hasara ya zaidi ya Sh3 bilioni.
Mtoto wa marehemu, Geofrey Kabwe, alisema baba yake alianza kuugua maradhi ya tumbo Julai mwaka jana.
Alisema Ilipofika Desemba, alizidiwa na familia iliamua kumpeleka India kwa matibabu zaidi.
“Alipofika India waligundua kuwa alipata hitilafu ndogo kwenye ini, hivyo akafanyiwa upasuaji, madaktari India walisema chanzo cha tatizo hilo ni dawa alizokuwa akitumia,” alisema Geofrey.
Alisema mwishoni mwa Januari, mkurugenzi huyo alirejea nchini akiwa na afya njema na alianza kwenda kazini Februari huku akihudhuria kliniki katika Hospitali ya Apollo nchini India.
Lakini kadri siku zilivyozidi kwenda, hali yake kiafya ilianza kuzorota na ilifikia hatua familia ilitakiwa kukutana ili kushauriana kuhusu hali hiyo.
“Wiki mbili zilizopita nilipigiwa simu nikiwa Arusha nikaelezwa kwamba hali yake kiafya siyo nzuri, tulimwona daktari wake na akabainika kuwa na Pneumonia (homa ya mapafu), akapewa dawa na sindano,” alisema Geofrey na kuongeza:
“Baadaye tulimpeleka TMJ kwa ajili ya kipimo cha CTScan, jana mchana majibu yalitoka yakionyesha kuwa ini lilikuwa limeharibika na tayari mwili ulikuwa umeanza kuvimba. Ilipofika saa mbili usiku hali ilibadilika akawa anakoroma na saa tatu usiku akafariki dunia,” alisema Geofrey.
Taarifa zilizopatika jana zimeeleza kuwa Kabwe amekuwa nje ya ofisi yake tangu alipoanza matibabu na siku ya kwanza kurejea kazini ilikuwa Aprili 19 ambako alikutana na rungu la Rais John Magufuli.
Msemaji wa familia, Dk Ez Machuve alisema mipango ya mazishi inaendelea: “Atasafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani kwake Jumanne jioni baada ya kuagwa hapa nyumbani kwake. Mazishi tunatarajia kufanya kijijini Mamba Mpinji Jumatano.”
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema katika kipindi chake cha kufanya kazi, hakubahatika kushiriki kazi yoyote na Kabwe kutokana na hali yake kiafya.
“Sikubahatika kufanya naye kazi, baada ya Rais kufanya uamuzi mgumu, aliondoka hivyo sikuwahi kushiriki naye,” alisema Mwita.
Kilichomwondoa kazini
Makosa yaliyosababisha Kabwe kusimamishwa kazi ni madai ya kusaini mkataba kwa kutumia sheria ndogo ya mwaka 2004 kutoza magari yanayotoka kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) Sh4,000 huku akidaiwa kusaini mkataba mwingine wa Sh8,000 chini ya sheria ndogo ya mwaka 2009.
Pia, madai ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa UBT hasa kwenye utaratibu wa kutoa magari na kukodisha vyumba vya kupangisha kinyume na taratibu na kuongeza muda wa mzabuni iliyeingia mkataba na jiji wa maegesho ya magari kinyume na taratibu.
Post a Comment