Mahakama ya Wilaya ya Chato Mkoani Geita imemtia hatiani Mgambo wa Mahakama ya mwanzo Buseresere Bw. Majaliwa Revelian Gwakilala kwa makosa ya kuomba na kupokea Rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1 na 2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Kwa Mujibu wa Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kesi dhidi ya Mtuhumiwa huyo ilifunguliwa mnamo tarehe 14/1/2016.
Akisoma hukumu mbele ya mwendesha mashitaka wa TAKUKURU Augustino Mtaki, Hakimu Hakimu Mfawidhi wa Wilaya hiyo Mh. Mh. Jovith Kato alisema kuwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mwendesha Mashitaka umethibitisha pasipo shaka yoyote kuwa Mtuhumiwa alitenda kosa hilo.
Ilisisitiza Sehemu ya Taarifa hiyo kuwa kwa mujibu wa ushahidi Mtuhumiwa aliomba kiasi cha Tshs. 300,000/= na kupokea kiasi cha Tshs. 100,000/- kutoka kwa Bw. Reuben Francis Ndimila ili asimkamate mtuhumiwa aliyeruka dhamana.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Mahakama ilimtia hatiani Mtuhumiwa katika makosa hayo mawili ya kuomba na kupokea hongo.
Aidha Mh. Kato akitoa adhabu kwa Mshitakiwa alisema, Mshitakiwa anatakiwa kutumikia kifungo cha miaka Mitatu (3) jela au kulipa faini ya Tshs. 600,000/= kwa kila kosa. Mshitakiwa amepelekwa jela kuanza kutumikia adhabu hizo kama zilivyotolewa. Kesi hiyo ilisajiliwa mahakamani hapo kama kesi ya Jinai Na. 18/2016 na kusikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa Wilaya hiyo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa GEITA Bw. Thobias Ndaro ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Chato kutoa taarifa mbalimbali za vitendo vya Rushwa na ubadhilifu katika miradi mbalimbali ya maendeleo na maeneo mengineyo ili watuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Post a Comment