Serikali imesema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 itatekeleza mradi wa maji katika vijiji 100 vilivyo pembezoni mwa bomba kuu la maji linalotoka ziwa Victoria hadi Kahama na Shinyanga ili kuwawezesha wanachi wanaoishi katika vijiji hivyo kupata huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza Bungeni mjini Dodoma leo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema kuwa mradi wa kuvipatia maji vijiji hivyo utakwenda sambamba na uboreshaji wa huduma ya maji kwenye vijiji 40 vilivyotambulika katika Halmashauri za Misungwi, Kwimba, Shinyanga na Msalala.
Amesema kazi ya kupima na kufanya usanifu wa miradi katika katika vijiji hivyo vya Halmashauri ya Msalala na Shinyanga imeanza na gharama yake imekadiriwa kufikia shilingi bilioni 2.59 huku akiongeza kuwa hadi machi, 2016 ujenzi wa miradi ya maji umekamilika katika vijiji 11 vya Halmashauri hiyo.
Mhe.Lwenge amesema katika mwaka wa bajeti 2016/2017 Wizara yake itakamilisha ujenzi a miradi ya maji katika Halmashauri za wilaya za msalala na Shinyanga na kuanza Usanifu wa miradi hiyo kwenye Halmashauri za Kwimba na Misungwi ambapo kiasi cha shilingi milioni 760.67 kimetengwa kwa kazi hiyo.
Amevitaja baadhi ya vijiji ambavyo sasa wananchi wake wanapata maji safi na salama kufuatia kukamilika kwa miradi hiyo kuwa ni Nyashimbi, Magobeko, Kakulu, Butegwa, Ngihomango, Jimodoli, Kadoto,Lyabusalu ,Mwajiji Ichongo na Bukamna.
Katika hatua nyingine Mhe.Lwenge amesema Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 kwa kushirikiana na Serikali ya Ubelgiji itatekeleza mradi mkubwa wa maji utakakaowawezesha wananchi Laki mbili (200,000) wa Halmashauri zote za mkoa wa Kigoma kupata maji safi na salama.
Amesema mradi huo unatarajia kugharamia kiasi cha Euro milioni 8.8 ambapo kati ya fedha hizo Euro milioni 8 zitatolewa na Serikali ya Ubelgiji na fedha iliyobaki itatolewa na Serikali ya Tanzania.
Ameongeza kuwa vijiji 26 vya kipaumbele vya mkoa wa Kigoma vimeainishwa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi na kuongeza kuwa wizara yake tayari imeshatenga kiasi cha shilingi bilioni 5.28 zote zikiwa ni fedha za nje kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Pia amesema Serikali katika mwaka wa 2016/2017 wa fedha imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1 kufanyia ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya maji ili kuzipatia maji kata saba za wilaya ya Masasi zenye idadi ya watu 84,082.
Aidha, amesema katika mwaka huo wa fedha serikali itatekeleza mradi wa kutoa maji mto Ruvuma kuyapeleka Mtwara –Mikindani pamoja na vijiji 26 vitakavyopatikana kilometa 12 kutoka eneo la bomba kuu.
Mradi huo utatekelezwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Jamhuri ya China kwa gharama ya dola za Kimarekani milioni 189.9 ambapo kazi ya ujenzi wa chanzo kutoka mto Ruvuma , Chujio la kutibu maji , nyumba ya kusukuma maji , matanki 26, tanki kuu la ujazo wa lita milioni 30 litakalojengwa eneo la maghamba.
Aidha, vituo vya kuchotea maji 234 na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji umbali kilometa 63 yatajengwa ili kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 9 hadi lita milioni 120 kwa siku ili kutosheleza mahitaji ya watu na viwanda mbalimbali vinavyojengwa vikiwemo vya Saruji na Gesi.
Post a Comment