Dodoma. Mbunge wa Simanjiro (Chadema), James Ole Millya amepelekwa katika Kamati ya Kinga, Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge baada ya kuwasilisha ushahidi wake wa kuhusu ushemeji wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama na mmoja wa wabia wa kampuni ya Sky Associates inayomiliki mgodi wa TanzaniteOne.
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema jana kuwa Millya aliwasilisha ushahidi wake na tayari umepelekwa katika kamati hiyo kufanyiwa kazi.
Millya alitoa tuhuma dhidi ya kampuni hiyo akieleza kuwa inalindwa na baadhi ya mawaziri huku akilitaja jina la Mhagama kuwa ana ushemeji na mmoja wa wabia, jambo linalowapa kiburi cha kufukuza watu bila kuchukuliwa hatua.
Mhagama aliomba mwongozo wa Spika kutaka Millya athibitishe aliyoyasema au afute kauli yake kwa mujibu wa kanuni za Bunge.
Akitoa majibu ya mwongozo ulioombwa na Mhagama, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema Millya alitoa madai hayo wakati akichangia hotuba ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Akinukuu maneno ya Millya kama yalivyo kwenye hansard alisema: “Na sheria za kazi zinajulikana ni bahati mbaya kwamba mama yetu Mhagama naye anatajwa kwamba ni shemeji wa mmoja wa mbia wa hapo. Dada anaitwa Asia Gonga ameolewa na Martin Mhagama au Yusufu Mhagama.”
Alipotakiwa kufuta au kuthibitisha kauli yake, Millya alisema ni kweli alitaja jina la Mhagama, lakini akaeleza kuwa alisema ametajwa na ana ushahidi wa watu wanaomtaja kwenye ujumbe wa simu.
Loading...
Post a Comment