Marehemu James Peter Nsemwa ‘Kinyambe’ enzi za uhai wake.
DAR ES SALAAM: WAKATI mwili wa msanii wa vichekesho James Peter Nsemwa maarufu kama Kinyambe ulitarajiwa kuzikwa jana katika Makaburi ya Uyole mkoani Mbeya, gazeti hili limefukunyua na kuupata undani wa kifo chake.
Kwa mujibu wa baba wa marehemu, mzee Lugendelo Nsemwa, mwanaye aliyejipatia umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa uchekeshaji, alianza kuumwa tangu Juni mwaka jana, ambapo tumbo na miguu ilikuwa ikijaa maji. Alisema tatizo hilo lilisababisha mapafu yake kushindwa kufanya kazi sawasawa.
Jeneza lenye mwili wa marehemu Kinyambe.
Katika hali ya kushangaza, mzazi huyo alisema jina la Mohamed Abdalah, ambalo linafahamika kwa wengi kama ndilo halisi la msanii huyo, yeye halitambui, kwani tangu amezaliwa alipewa jina hilo na hakuwahi kusikia kama alilibadili.
Aidha, aliwalaumu wasanii wenzake kwa kutotoa msaada wowote wakati wa ugonjwa, kwani kwa kipindi chote hakuwahi kuwaona wasanii wa Dar es Salaam wala kupata salamu zao, zaidi ya kuwaona wale wa Mbeya ambao nao walikuwa wakienda mara mojamoja.
Daktari mmoja wa hospitali hiyo aliyemhudumia marehemu tangu alipolazwa, ambaye jina lake linahifadhiwa kwa kuwa siyo msemaji wa hospitali hiyo, alisema marehemu alipopokelewa na kupimwa, aligundulika kiwango cha sukari kuwa chini huku pia akiwa na homa ya mapafu.
Wakati wa uhai wake, Kinyambe aliwahi kuishi na wanawake watatu, ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja, lakini imefahamika kuwa wa kwanza alizaa naye mtoto mmoja, wa pili alizaa naye mtoto mmoja pia, lakini alifariki mwezi uliopita akiwa na miaka minne. Mwanamke wake wa mwisho ni mjamzito ambaye endapo Mungu atamjaalia, atajifungua mwezi ujao.
Marehemu alijipatia umaarufu kwa vichekesho vyake kupitia vipindi mbalimbali vya televisheni, kikiwemo cha Vituko Show katika Channel Ten na pia aliwahi kufanya kazi na Sharo Milionea.
Mungu ailaze Roho ya marehemu mahali pema peponi!
Post a Comment