Rais John Magufuli
Katika kipindi hicho cha siku 180, Dk Magufuli ametangaza kubana matumizi serikalini, kuongeza ufanisi katika utumishi wa umma kwa kutumbua watumishi wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu na uzembe huku akidhibiti ukwepaji kodi uliokuwa umeshamiri nchini.
Sehemu kubwa ya mikakati hiyo inayoendeshwa na kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ imepokewa kwa mikono miwili na wananchi huku baadhi wakionyesha wasiwasi kuwa yapo baadhi ya masuala yanayotakiwa kuwekewa mkazo au kurekebishwa ili kuzuia madhara siku zijazo.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama huru vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholas Mgaya alisema utendaji wa Rais Magufuli kwa miezi sita ya awali unaridhisha “kwa kiasi fulani” katika jitihada za kuwaletea Watanzania maendeleo.
Hata hivyo, Mgaya alisema kuna maeneo ambayo hayajaguswa ipasavyo kama sekta ya elimu, afya na Serikali za Mitaa ambako kuna viongozi wachache wanaotumia nafasi zao kuwanyanyasa wananchi na watumishi na kufanya ubadhirifu wa mali ya umma.
“Huko ndiko kuna uozo mkubwa na Watanzania wengi wanaishi kwenye halmashauri za wilaya, miji na majiji. Rais aweke nguvu kutumbua viongozi miungu watu,” alisema Mgaya.
Katika miezi yake ya awali Ikulu, Rais amekuwa katika kampeni kali ya kubana matumizi ambayo imekwenda sambamba na ufutaji wa safari za nje kwa watumishi wa umma mpaka kwa kibali maalumu akisema kuwa ni “mzigo kwa Taifa”.
Ubanaji huo wa matumizi ulihusisha upigaji marufuku taasisi za umma kutumia kumbi za kukodi kufanyia mikutano na badala yake kutumia majengo ya Serikali, jambo ambalo limepingwa na baadhi ya wachumi.
Honest Ngowi, Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema kubana matumizi yasiyo ya lazima ni jambo jema lakini ubanaji huo ukifanyika kuzidi kiwango huleta madhara kiuchumi kwa kuwa Serikali inahimizwa kutumia ili kuchochea maendeleo.
“Serikali ni mlaji mkubwa mahali popote ulimwenguni. Wasibane matumizi kupitiliza, uchumi utasinyaa,” alisema.
Hata hivyo, alisema Dk Magufuli amefanya vyema zaidi katika kudhibiti ukwepaji kodi katika maeneo mbalimbali hususan bandarini ambako hali ilikuwa mbaya.
Katika kuhahikikisha nyumba inakuwa safi, Dk Magufuli alianza utawala wake kwa utumbuaji majipu ambao umeshuhudia vigogo wa mashirika makubwa nchini kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) wakisimamishwa kupisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi.
Hata hivyo, utumbuaji huo umeonekana kukubalika na wengi lakini baadhi wamepinga staili ya watumishi hao wanavyotumbuliwa ikiwamo kuuliza wananchi kama mtumishi anafaa kutumbuliwa au la kama alivyofanya Rais wakati akimtumbua aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe wiki mbili zilizopita.
“Hawa wanaotumbuliwa wakienda kwenye vyombo vya sheria na kushinda kesi, Serikali italipa fedha nyingi. Huo utumbuaji wa majipu ni mzuri katika kurudisha nidhamu serikalini lakini ni vyema ukazingatia sheria,” alisema Mgaya.
Rais Magufuli amekuwa akieleza kuwa Serikali yake imelenga kuipeleka nchi kuwa na kipato cha kati kwa kukuza sekta ya viwanda na kilimo ili kuongeza ajira na uzalishaji.
Mkurugenzi wa asasi ya kiraia ya Fordia, Buberwa Kaiza alisema hadi sasa utawala wa Rais Magufuli una mwelekeo mzuri katika usimamizi wa kiuchumi lakini amekosa sera kuu ya uchumi.
“Kueleza kuwa nchi ya viwanda ni sawa lakini mwelekeo wa uchumi ndiyo unasaidia kwa sababu viwanda hivyo havijengwi na Serikali, bali wawekezaji,” alisema Kaiza.
Kuhusu utendaji wa Serikali kwa ujumla, Kaiza alisema Rais Magufuli anaipeleka nchi katika mwelekeo mzuri kwa kuwa ameitoa kwenye ngazi hasi hadi sasa ambako ufanisi umeanza kuonekana katika utumishi wa umma.
Alisema kuna madhara ya muda mfupi ya kiuchumi kutokana na ubanaji matumizi na ukwepaji kodi lakini ni bora kuliko kuwa na kampuni inayosaidia ukuaji uchumi kwa kuajiri wengi kwa njia zisizo halali.
Lakini wakati utawala wa Rais Magufuli ukipigiwa chapuo katika miezi sita ya awali, sakata la kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge limeanza kuonyesha kuwa huenda Serikali yake ikafanya vibaya kwenye masuala ya utawala bora.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shumbusho Damian alisema mikakati ya Rais kuirudisha nchi kwenye mstari ni mizuri lakini utawala bora utashuka iwapo wananchi wananyimwa uhuru wa kujieleza na kupata habari.
“Unaweza kufanya maboresho ya kila aina nchini kwa kutoa huduma bora lakini usishawishike kudhibiti uhuru wa kujieleza,” alisema.
Pia, alionyesha wasiwasi kuwa utumbuaji majipu unajenga nidhamu ya woga kwa kuwa watumishi wengi wanafanya kazi kwa kuhofia kufukuzwa bila ya kuwa ari ya kuwahudumia wananchi.
Post a Comment