NA BASHIR NKOROMO
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeonya vikali juu ya mkakati wa viongozi wa UKAWA, wa kufanya ziara mikoani, katika kile ambacho wanakiita ni kwenda kuishitaka serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli kwa wananchi.
Aidha CCM kimesema, daima hakitavumilia juu ya jambo lolote ambalo litaonekana kuwa na nia ovu ya kumchafua Rais Dk. Mafuli na kitakula sahani moja na UKAWA katika kampeni hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, jana, Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, alisema, wamesikitishwa na kauli zinazotolewa na wapinzani ya kupinga kasi ya Rais Dk. Magufuli hususan katika dhama yake ya utumbuaji majipu, kubana bajeti na matumizi ya serikali pamoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za wananchi katika sekta mbalimbali.
Sendeka alisema, upo mkakati mchafu ambao wapinzani wamekuwa wakipanga kwa nia mbaya ya kutaka kuchafua taswira ya Rais Dk. Magufuli , mkakati ambao amedai hauwezi kuungwa mkono na wananchi.
Alisema, tangu Mei 16 mwaka huu baada ya Kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA, habari za mwanzo zilianza kuandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari juu ya yaliyojiri katika mkutano huo.
Alisema, mkakati huo unaegemea katika kuandaa umma kwa kile kinachoitwa kwenda kumshitaki Rais Dk. Magufuli kwa wananchi.
“Kwamba Serikali ya Rais Dk. Magufuli inaidaiwa kuendesha nchi kifashist na inalenga kuipeleka nchi katika utawala wa kidikteta ambao haujazoeleka katika nchi yetu,”alisema Sendeka.
Alisema, kipindi cha nyuma moja ya mambo ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele na vyama vyote ni ufisadi, rushwa na suala la serikali kutokuwa na maamuzi, ambapo baada ya uchaguzi mkuu uliopita, baada ya Rais Dk. Magufuli kuchaguliwa amesimama kidete kupambana na mambo hayo licha ya kwamba yapo katika, ilani , sera za msingi na kiapo cha uanachama cha CCM.
“Wenzetu mara baada ya kumpata mgombea wao (Edward Lowassa), ujasili wa kuzungumzia rushwa na ufisadi ulipungua. Kwa sababu ambazo kila mtanzania anajua kwamba ni kwanini wamekosa utashi wa kuendelea kulikemea suala hilo la rushwa , ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma,”alisema Sendeka.
Alisema, baada ya Rais Dk. Magufuli, kuingia Ikulu, mapambayo dhidi ya mambo hayo ameyafanya kwa kasi ya aina yake, ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya rushwa, kuziba mianya ya upotevu wa fedha za serikali, kubana matumizi kwa kufuta bajeti kubwa za Sikukuu, kufuta safari za nje pamoja na wakati mwingine kuelekeza fedha katika maeneo ambayo yanamatatizi makubwa.
Alise, Rais Dk. Magufuli alichokuwa anafanya ni kumalizia ngwe ya mwisho ya bajeti ya mwaka wa fedha 2015/16 na kwamba atafanya vizuri zaidi baada ya bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17 kupitishwa.
“Katika mapambano hayo, ambayo rais ameyafanya kwa utashi mkubwa, tunajua kwamba yamegusa watu wengi . Hakuna mashaka kwamba katika nchi hii tayari kuna watu ambao wametengeneza utajiri wa muda mfupi ambao unatia ukakasi unaoweza kumuudhi mtu yoyote mwenye mapenzi na nchi hii,”alisema Sendeka.
Alisema utendaji huo ulifanya kupokea sifa nyingi zilizoelekezwa kwa Rais juu ya utendaji wake, lakini baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA, walibaini wazi bila mashaka kwamba anayoyafanya Rais Dk. Magufuli yanapandisha chati ya CCM kwenda juu. Kwa sababu serikali iliyopo madarakani ndiyo inayokijengea chamas uhalali na uhalali wa chama chochote unsajengwa na utendaji wa serikali iliyopo madarakani.
“Serikali iliyopo madarakani isipo tekeleza matarajio ya wananchi, uhalali wake haupo. Vitendo vya Rais Dk. Magufuli, hakuna mashaka kwamba watanzania wameunga mkono na Dunia imeunga mkono. Hata umoja wa mataifa kupitia Shirika la Maendeleo (UND) imeunga mkono uwajibikaji huo, katika mapambano ya rushwa , ukusanyaji mapato na nidhamu ya uwajibikaji kwa watumishi wa umma,”alisema Sendeka.
Alisema, inashangaza kuona kwamba CHADEMA wanadai suala la kupambana na rushwa na ufisadi Rais Dk. Magufuli amepora kwao na kusahau kwamba , ajenda hiyo ilikuwa ni ya CCM na TANU.
“Kilicho fanyika ni kumpata kada ambaye anaweza kusimamia na kutekeleza hayo, jambo ambalo limeanza kuwafanya wapinzani kuamini kwamba itaua upinzani, na kwamba hofu yao ni uwezekano wa kupoteza wabunge wengi katika uchaguzi mkuu wa 2020 ni mkubwa,”alibainisha msemaji huyo.
Alisema baada ya kufanya tathimini hiyo ndipo walipokubariana kwenda kwa wananchi wakiwa na ajenda ya kupotosha umma juu ya utendaji wa Rais Dk. Magufuli na serikali yake.
“Walianza na kampeni ya rais ya utumbuaji wa majipu na wao kupitia kwa mgombea wao wa urais Lowassa kisha kwa mwenyekiti wa CHADEMA , Freeman Mbowe, walikemea ajenda hiyo kwamba inaukiukwaji wa haki za binadamu.
Kwamba unapokwenda bandarini nakukuta makontena 2000 au 3000 hayajalipiwa kodi unamuacha huyo Kamashna na wasaidizi wake na kwamba hiyo ndiyo haki ya binadamu?” alihoji Sendeka.
Alisema viongozi hao pia waliponda kwamba serikali ya Rais Dk. Magufuli inatanguliza vitendo kuliko fikra.
“Hivi jamani, umemkuta mtu na kila dalili za kufanya ufisadi, unamuacha na kuanza kufikiria jambo la kufanya.
Serikali ya Magufuli inasema kaa pembeni, jitetee kisha hatua zaidi zinachukulia .Hii ni kwa nia njema ya kueta maendeleo ya nchi kwa kutumia vyanzo vya mapato yetu, kutoa huduma muhimu zinazostahili kwa wananchi.
Na kazi hiyo ameifanya kwa ufanisi mkubwa kwa muda mfupi aliokaa katika uongozi,”alibainisha Sendeka.
Aliongeza “Sasa haya yamewaudhi. Walijaribu kupima kina cha maji wamebaini kwamba hawayawezi na wamebaini kwamba watanzania wote wamechoka na wanaunga mkono hatua hizi za rai,”
Sendeka alishangazwa na wapinzani kulalamikia hatua ya Rais Dk. Magafuli kutumbua majipu kwamba ni udikteta na ufashisti wakati rais ania njema ya kutetea wanyonge na maslahi mapana ya taifa.
Alisema binafsi anamuunga mkono Lowassa kwa kauli yake aliyoitoa hivi karibuni kwamba, kazi yake kubwa sasa ni kukigeuza CHADEMA kutoka kuwa katika kikundi cha wanaharakati na kuwa chama kamili.
“Najiuliza kama miaka 20 zaidi ya uwepo wa CHADEMA hakikuweza kubadilika kutoka katika kikundi cha wanaharakati mpaka Lowassa alipo kikuta na kutaka kukibadilisha ndani ya miaka minne ijayo kiweze kuwa chama kamili cha siasa nina uhakika muda huo hautoshi,” alisema Sendeka.
Aliongeza, ”Lakini najiuliza kama Magufuli anatumbua majibu wapinzani wanadai ni dikteta na fashist. Magufuli anaziba mianya ya rushwa wanachukia. Najiuliza wametumwa nanani? Kumwakilisha nani? Kutetea maslahi ya nani? Na nani kawafadhili?
”
Alisema ni dhahiri anayetetea ufisadi anawasemea waliotumbuliwa na ambao mianya yao ya rushwa imezibwa.
Sendeka alisema, wakati ufusadi ulivyo kuwa ukifanyika katika sekta muhimu, wapinzani hawakuacha Bunge wala vikao na kwenda kuitisha mikutano kwa wananchi na kuwaambia kwamba bandari na TRA kuna ufisadi.
“Wakati wa kashfa ya ukwepaji wa kodi ya sukari hakuna aliyetoka kwenda kwa wananchi kuitisha mikutano au kuingia barabarani kuandamana kwa sababu kodi haijalipwa. Wakati wa kashfa ya Escrow, hakuna chama kilicho funga safari kwenda mikoani kuitisha mikutano na kuwaeleza wananchi kwamba kuna ufisadi huo,”alisema Sendeka.
Alisema, inshangaza kuona wakati serikali inajitahidi kupambana na changamoto zinazowakabili wananchi, wapinzani wanajipanga kwenda mikoani kupinga hatua hizo kwa kile wanachokiita kushtaki serikali kwa wananchi.
.
“Dhamira ya wenzetu sasa ni kujitahidi kutumia nguvu zao na zawale wanaowatuma kuchafua jina la Dk. Magufuli bila kuelewa kwamba Watanzania hasa wanyonge wataendelea kutumia jina la Rais huyu kama alama kuu na muhimu , katika mapambano dhiti ya ukiritimba, ufisadi, na viongozi na watendaji wanaokubali kufanya kazi ya ukuwadi kwa manufaa yao binafsi huku wakiyaweka pembeni maslahi ya taifa,” alisema Sendeka.
Alisema CCM haipingi ziara hizo za viongozi, lakini daima hakitavumilia ikiwa mikutano yao italenga katika kumchafua rais.
“Wakijaribu kuchafua rais, watakapo CCM nayo itakanyaga pia. Watakapo ondoa mguu wao nasisi tunaweka mguu wetu ili kuwaeleza ukweli wananchi juu ya kazi kubwa inayofanywa na serikali. Tunawasemaji wengi na tunauwezo wa kufika popote,” alisema Sendeka.
Aliongeza, ”Watanzania watapima, kauli ya watu wanaotetea mafisadi, wakwepa kodi na wala rusahwa na CCM inayotetea wananchi wanyonge ili waweze kufaidi matunda ya nchi yao,”
Alisema, kama hoja zao ni hizo, za kumchafua Rais Dk. Magufuli CCM inawaonea huruma, na wasifiriki watanzania walio timamu watawaunga mkono.
“Siyo tu kwamba watanzania hawatawaunga mkono, bali watawashangaa na heshima yao itashuka. Watanzania wanaakili, hawawezi kutetea wezi wakati rais anafanya kazi nzuri ya kuwatetea,”
Post a Comment