Dar es Salaam.
Madereva wa magari, bodaboda na bajaji wanaovunja sheria na kuyasababishia ajali ya Mabasi ya Mwendo Kasi (Udart) watatozwa faini isiyopungua Sh300,000.
Meneja Uhusiano wa Dart, William Gatambi alisema wamewasilisha maoni ya kupitishiwa sheria ndogondogo kwa ajili ya barabara zinazotumiwa na mabasi hayo katika wizara husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
“Sheria hizo zitawabana madereva ambao wamekuwa wakipuuza taratibu na matumizi sahihi ya miundombinu, suala ambalo limekuwa likisababisha ajali za kila siku na usumbufu kwa madereva wa mabasi hayo,” alisema Gatambi.
Aliongeza kuwa mchakato huo uko katika hatua za mwisho kukamilika na baadhi ya sheria hizo zinaambatana na adhabu ya faini ya kuanzia Sh300,000 na kuendelea, kushikiliwa kwa chombo kilichosababisha ajali kwa muda na kifungo gerezani.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Udart, David Mgwassa alisema mabasi 34 yalipata ajali katika kipindi cha siku 20 tangu kuanzishwa kwa mradi huo.
Mgwassa alisema gharama ya kuyatengeneza mabasi hayo ni kati ya Sh2.5 milioni hadi Sh3.5 milioni kwa kila moja.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga alisema takwimu zao zinaonyesha kwamba zimetokea ajali 13 zikihusisha mabasi hayo tangu Mei 10.
Licha ya ajali, mradi huo wa awamu ya kwanza wa Udart umekumbwa na changamoto nyingine ikiwamo ugumu katika upatikanaji wa tiketi kwa abiria.
Loading...
Post a Comment