Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amewataka Watanzania kujali makundi ya watu wenye mahitaji maalumu hususan katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Kauli hiyo aliitoa jana alipotembelea vituo vya watoto yatima jijini Dar es Salaam vinavyoendeshwa na Waislamu kwa lengo la kuwajenga watoto kiimani. Lengo la ziara yake ni kushiriki nao katika utekelezaji wa nguzo ya mfungo wa Ramadhan.
Katika ziara hiyo, Lowassa aliyekuwa ameongozana na waumini mbalimbali wa dini hiyo, alitembelea vituo vitatu vya yatima ambavyo ni Chakuwama kilichopo Sinza, Khairat cha Kigogo na Umra kilichopo Magomeni Mwembechai.
Katika ziara hiyo, Lowassa alitoa msaada wa unga, mchele, mafuta ya kupikia, tende na sukari.
Lowassa alitoa rai kwa watu wenye uwezo kujiweka karibu na jamii inayohitaji msaada, ili kuenzi utamaduni wa Watanzania kusaidiana. “Jamii lazima tuangalie makundi haya kwa kushiriki nao pamoja kwenye mahitaji yao, kula nao pamoja,”alisema.
Mratibu wa misaada hiyo, Sheikh Rajab Katimba ambaye ni Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, alisikitishwa na baadhi ya Waislamu wanaofuturisha makundi ya watu wenye uwezo na kusahau makundi ya wasiojiweza.
“Tusaidiane Waislamu na inashangaza sana kuona jamii inayohitaji msaada inasahaulika na kufuturisha wenye kujiweza kiuchumi, siyo mbaya ila tukumbuke jamii hii yenye uhitaji,”alisema Sheikh Katimba.
Mbali na salamu hizo, dua zilisomwa na watoto wawili, Fadhia Liziki (3) na Nasra Ramadhan (3) wa kituo cha Kigogo kuombea amani.
Asnat Ali (6) wa kituo hicho alitoa shukrani zake, huku akihitaji ukarimu huo uguse kundi la Watanzania wengine walio na nafasi ya kiuchumi. Saida Hassan ambaye ni mmiliki wa kituo cha Sinza chenye watoto 90, alishukuru misaada hiyo huku akiomba ushirikiano zaidi wa kulea watoto hao.
Post a Comment