MKamishna Mkuu wa TRA Bw. Alphayo Kidata akitilia mkazo jambo wakati wa kikao na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya makusanyo ya mapato kwa mwezi Mei 2016,kilichofanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro, Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo na kushoto ni Meneja wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Abdul Mapembe.
MAMLAKA ya Mapato Tanzania imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 1.032 katika mwezi Mei ambayo ni sawa na asilimia 100.7 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.025 katika mwezi huo.
Makusanyo ya kipindi cha miezi kumi na moja (Julai 2015 hadi Mei 2016) ni jumla ya shilingi trilioni 11.956 sawa na asilimia 99.2 ya lengo la shilingi trilioni 12.054 katika lengo la kipindi hicho kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi leo kuhusu mwenendo wa makusanyo ya mapato, Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Alphayo Kidata amesema TRA inaendelea na jitihada mbalimbali kuhakikisha inafikia na kuvuka lengo la makusanyo iliyopangiwa na serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 na kuendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili Mamlaka katika ukusanyaji wa mapato.
“TRA imejiwekea mikakati thabiti ya kuongeza mapato kwa kipindi cha mwezi mmoja uliobaki ili kuweza kufikia au kuvuka lengo kwa mwaka huu wa fedha, ambapo kwa sehemu kubwa tumeendelea kupambana na magendo hususani katika pwani ya bahari ya Hindi na mipaka yote, kupambana na wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi na wanaokiuka kutumia mashine za kodi za keielektroniki , kuwawajibisha wafanyakazi wasio waadilifu pamoja na kuhakikisha inaboresha zaidi mifumo itakayompa urahisi mlipakodi katika zoezi zima la ulipaji kodi wa hiari, alisema Kamishna Mkuu.
Bw. Kidata ameendelea kusisitiza wananchi na wafanyabiashara kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa kutoa na kudai risiti za EFD pindi wanaponunua au kuuza bidhaa pamoja na huduma ili kuongeza mapato ya nchi.
Katika kutekeleza agizo la Mh. Rais na kuhakikisha wafanyabiashara wanatoa ushirikiano katika matumizi ya mashine za EFD Mamlaka imeanza utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ugawaji wa mashine za EFD kwa wafanyabiashara wadogo kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
TRA imeanza ugawaji wa mashine za EFD kwa wafanyabiashara wapatao 5,703 wenye mauzo ghafi kati ya Shilingi milioni 14 na milioni ishirini (20) kwa mwaka, wafanyabiashara hao wanatakiwa wafike katika ofisi za Mamlaka ya Mapato za Mikoa wanayolipia kodi ya Ilala, Kinondoni na Temeke ili waweze kuhakiki usajili wao wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na kupewa kibali cha kupewa Mashine ya EFD zoezi lililoanza Juni Mosi alisisitiza Kamishana Mkuu.
Aidha, Bw. Kidata alifafanua kuwa zoezi hili litaendelea katika Mikoa yote Tanzania kwa awamu kwa utaratibu utakaotangazwa mara kwa mara na hivyo kutoa wito kwa wafanyabiashara wenye mauzo tajwa wote nchini kutoa ushirikiano pindi inapofika zamu yao katika Mikoa yao.
Zoezi hili litasaidia kuongezaka kwa Mapato ya nchi endapo wafanyabiashara na wananchi watakuwa bega kwa bega katika kuhakikisha wanatumia mashine hizo na kutoa taarifa kwa Mamlaka kuhusu wafanyabiashara wote watakao kiuka kutumia mashine hizo za EFD.
Kwa upande wa wananchi, kamshna mkuu amewaasa kuadai risiti kila wanunuwapo bidhaa au kupata huduma na kuhakikisha usahihi wa kiwango walicholipia sambamba na risiti walizopewa .
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu"
Imetolewa na:
Idara ya Huduma na Elimu kwaMlipakodi
Post a Comment