Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MASWALI MATANO MAGUMU JUU YA MAUAJI YA KINYAMA YA WATU


 Matukio ya mauaji ya watu wakiwamo viongozi wa serikali za vijiji na dini yanayoendelea nchini yamezidi kuwajengea hofu wananchi, huku yakiacha maswali kadhaa kutokana na kufanana kwake.
Katika matukio yote yaliyorekodiwa nchini katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, watu wasiojulikana wamekuwa wakitumia silaha kama visu, mapanga, na mashoka baadhi wakiwa na alama za kundi la IS.

Matukio yaliyotikisa nchi ni ya watu saba wa familia moja katika kijiji cha Sima Wilaya ya Sengerema kuchinjwa; watu watatu kuuawa katika msikiti wa Rahman Mtaa wa Utemini Kata ya Mkolani; na kuuawa Mwenyekiti wa kijiji cha Bulale Kata ya Buhongwa pia Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza. Mauaji mengine yaliyoishtua nchi ni ya watu wanane katika eneo la mapango ya Amboni, Tanga.

Ili kuhakikisha wahalifu wanapatikana wakiwa hai au wafu, Jeshi la Polisi lililazimika kutumia silaha nzito za kivita kukabiliana nao. Polisi hawajafanikiwa kukamata wauaji wa watu wanane Tanga, lakini usiku wa kuamkia Jumapili, Polisi mkoani Mwanza walifanikiwa kuvamia mapango yaliyoko katika mlima wa mawe Utemini na kuwaua watuhumiwa watatu wa uhalifu.

Akizungumzia tukio la Amboni, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Abdullah Luhavi alisema majibu yote yatapatikana baada ya oparesheni na akashauri vyombo vya ulinzi viachwe vifanye kazi yake.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akielezea mafanikio ya mapambano katika mapango ya Utemini alisema mkakati wa Serikali wa kufanya Mwanza kuwa sehemu salama umeanza na hakutakuwa na mhalifu atakayeingia na kutoka salama.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alisema jeshi hilo linaendelea na kazi yake na kwamba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu alishazungumzia mauaji hayo akiwa Tanga. “Tutatoa taarifa tena baadaye lakini kwa sasa tayari IGP alishazungumza,” alisema.

Maswali
Wananchi wanahoji maswali kadhaa jinsi matukio ya Mwanza na Tanga yanavyofanana kwa muda wa uhalifu, sababu, namna mauaji yanavyofanyika, vifaa vya uhalifu, wanakojificha na silaha zinazotumiwa na Jeshi la Polisi kupambana na wahalifu hao.

Kwa nini mauaji ya Tanga na Mwanza yalitokea baada ya watoto kukamatwa?
Katika tukio la Tanga, mke wa marehemu Mkola Said, Asha Said alisema wauaji walipofika nyumbani kwake walimuuliza mumewe: “Wako wapi watoto wetu mliowapigia simu polisi wakawachukua?”
Ilidaiwa kuwa siku chache kabla ya tukio hilo watoto nane wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 16 walipita kijijini hapo na kukamatwa, ingawa moja alikimbia.

Pia, mauaji ya watu watatu katika msikiti wa Rahman Mtaa wa Utemini akiwamo imamu Feruz Ismail yaliyofanyika Mei 18 ni baada ya watoto kukamatwa. Ilidaiwa siku chache kabla ya mauaji hayo, polisi walivamia na kuwakamata vijana kadhaa waliokuwa wakifanya mafunzo ya karate katika moja ya misikiti mitatu iliyoko Utemini.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema wauaji hao walikuwa wameshika bendera nyekundu iliyokuwa na maandishi meupe yaliyosomeka IS. Kadhalika shuhuda huyo alieleza kuwa kabla ya kuua walimuuliza Imamu:
Mfano huu wa tukio la Mwanza na la Tanga umezua maswali kwamba huenda wauaji hao ni wale wale au wenye lengo moja.

Kwa nini mauaji ya kuchinja yalifanyika saa 7.00 usiku?
Matukio mawili ya mauaji yalifanyika muda wa saa saba usiku. Tukio la kwanza lilitokea Mei 10 katika kijiji cha Sima Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, ambako watu saba wa familia moja waliuwawa kwa kukatwa mapanga.

Tukio linalofanana na hilo ni la mauaji ya watu wanane yaliyofanyika Amboni, Tanga Mei 28.
Kwa nini wamelenga viongozi?
Japokuwa hadi sasa haijulikani kwa dhati sababu za vifo vya watu hao, wauaji wa Amboni Tanga walilenga viongozi waliotoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kwenda kuwakamata watoto waliopita katika eneo hilo; mauaji ya Imamu Feruzi kwa madai ya kuendelea na ibada wakati wenzao wamekamatwa na pia aliuawa Mwenyekiti wa Bulale alipokuwa akisuluhisha wanandoa.

Kwanini wauaji wanajificha kwenye mapango?
Mara kwa mara wahalifu wanaofanya uhalifu Tanga, hukimbilia kujificha katika mapango ya Amboni na walioua waumini msikitini Mwanza walikwenda kujificha katika mapango jirani katika eneo la mlima wa mawe Ibanda Relini. Je, kuna usalama wowote katika mapango mengine nchini. Ni swali ambalo hakuna ofisa yeyote aliyekuwa tayari kujibu jana.

Kwa nini polisi walipambana na majambazi hayo kwa zaidi ya saa 14?
Katika mapambano dhidi ya wanaoitwa majambazi kule Amboni, polisi hawajafanikiwa kumkamata yeyote; mwaka jana mwanajeshi mmoja aliuawa, lakini hakuna jambazi aliyenaswa. Katika eneo la Utemini polisi wamepambana na kufanikiwa kuwaua watatu baada ya zaidi ya saa 14. Je, hao ni majambazi wa kawaida?

Kwa nini polisi wanatumia silaha za kivita?
Jeshi la Polisi mara zote huwa linadai linakabiliana na wahalifu wa kawaida, majambazi na vibaka lakini kinachowashtua watu ni matumizi ya silaha nzito za RPG za kudungulia ndege au kuharibu vifaru. Watu wanahisi wahalifu hao si wa kawaida na hapo kunazua maswali zaidi.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema kiuhalisia mauaji hayo yanatisha na kwamba yameleta sura tofauti.

“Wananchi wanachanganyikiwa na kujiuliza maswali mengi kwamba, mauaji haya ni ugaidi? Kiukweli mauaji haya yamesababisha taharuki kubwa miongoni mwa jamii,”alisema.
Alisema ipo haja kwa vikosi vyote vya usalama kuimarisha usalama wa raia na mali zao ili kuwanusuru na mauaji yanayoendelea kutokea wakati, vikosi hivyo vipo.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrick Ole-Sosopi alisema ni jukumu la Serikali kutoa majibu ikiwa matukio hayo ni ya kigaidi au la ili kuondoa hofu kwa jamii. “Inaogofya na kutisha kwa sababu bado tuna wasiwasi juu ya mauaji haya. Serikali ilikaa kimya hadi ilipoona matukio yanazidi kuwa makubwa. Tunachotarajia ni majibu yatakayosaidia kuwafanya wananchi watulie, kwa sasa bado kuna hofu,”alisema.

Sosopi pia alisema Serikali inatakiwa kuongeza bajeti kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuwezesha kazi za ulinzi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu ch Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema kwa kuwa matukio hayo huwa ni ya msimu, lazima suala la ulinzi na usalama wa raia liimarishwe.
“Siyo mara ya kwanza kwa Amboni kutokea mauaji haya, ni vizuri kuanzishwe kikosi cha jeshi ili kuwahakikishia usalama raia walioingiwa na hofu,”alisema.

Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Frank John alisema licha ya kuwa matukio hayo yanatisha, bado jamii haipaswi kukwepa jukumu la kusaidia ulinzi na usalama kwenye eneo lake, ikiwamo kutoa taarifa ya wageni wanaoingia na kutoka.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha vitengo vya intelijensia ili kukabiliana na uhalifu wa kimakundi. “Mambo haya yanayoendelea nchini tujue kuwa jamii yetu imeingia katika hali ambayo inatishia usalama wa wote si waislamu, wakristo au madhehebu mengine. Tuvisaidie vyombo vyetu,”alisisitiza.
Juzi, Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakary Zuberi aliitaka Serikali kuhakikisha inalinda amani na alilaani mauaji yanayoendelea .
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top