Bibi kizee alivyonaswa usiku akirandaranda na tunguri nyumbani kwa Waziri Mwigulu Nchemba.
DODOMA: Katika hali isiyo ya kawaida bibi kikongwe mmoja ambaye hakuweza kujulikana jina lake, amezua sintofahamu baada ya kukutwa nyumbani kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba akizunguka nyumba yake usiku huku akiwa na tunguri na wembe wenye damu
Tukio hilo lilitokea Mei 31, mwaka huu majira ya saa 6 usiku katika eneo la Kilimani mjini Dodoma kwenye nyumba ya waziri huyo ambako ni makazi ya mawaziri na viongozi mbalimbali wa umma.
Akizungumza na mwandishi wetu, eneo la tukio, shuhuda wa tukio hilo, Sumai Juma alisema kuwa alimwona mwanamke huyo akiwa amekumbatia vitu vyake akizunguka nyumba ya waziri.
nchemba1Baada ya kumwona mtu huyo, alilazimika kuita mlinzi na kujaribu kumhoji bila mafanikio kutokana na mwanamke huyo kutojua lugha yoyote na kila anachoulizwa alikuwa hajibu zaidi ya kurudia maneno yaleyale ambayo alikuwa akimuulizwa.
“Huyu kikongwe alikuwa kama na zaidi ya miaka 70 hivi, nilimwona akiwa amesimama katika dirisha la mheshimiwa waziri na baada ya kumfuata alianza kuzunguka nyumba hiyo asijue mlango wa kutokea…nyumbani hapa kuna uzio mrefu sana ambao bibi kama huyu hana uwezo wa kupanda na getini muda wote kuna walinzi wa Kampuni ya Moku Security ambao hawakumwona akiingia getini hapo,” alisema Juma.
Hata hivyo, alisema baada ya kumkamata walichunguza mzigo aliokuwa amebeba ambao ulifungwa katika kanga, kulikuwa na kuni kama 17 hivi, kikopo chenye vitu kama ungaunga mweusi mfano wa vumbi, mkaa na wembe aina ya Topaz uliokuwa haujafunguliwa ila ulikuwa umelowa damu.
Juma aliongeza kuwa, baada ya kumkagua na kutokana na mtu huyo kutojitambua, walilazimika kumpeleka Kituo cha Polisi Dodoma ambako walimweka mahabusu baada ya kushindwa kujieleza na asubuhi Waziri Nchemba alilazimika kwenda kuruhusu kuachiwa huru baada ya kumsamehe.
Kwa upande wake Waziri Nchemba alisema ameshindwa kujua lengo la mwanamke huyo katika nyumba yake lakini yeye hana hofu yoyote kwani yupo kwa ajili kuwatumikia wananchi kwa nafasi yake ya uwaziri na hivyo kazi yake anayoifanya anaiweza kwa kuwa anamtanguliza Mungu mbele.
Hata hivyo, alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuliombea taifa kwani kazi kubwa ambayo serikali ya Rais Dk. John Pombe Magufuli inayofanya ni tunu kubwa ya nchi yetu.
Loading...
Post a Comment