Na: Veronica Kazimoto
Dar es Salaam
10 Juni, 2016.
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Mei, 2016 umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 5.2 kutoka asilimia 5.1 ilivyokuwa mwezi Aprili, 2016.
Hii inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2016 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2016.
Kwa mujibu wa wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa iliyotolewa leo Jijini Dar es Salaam, kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Mei, 2016 kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja na mahindi kwa asilimia 1.5, unga wa muhogo kwa asilimia 6.2, nyama ya kuku kwa asilimia 2.6, njegere kwa asilimia 5.8, mihogo mibichi kwa asilimia 8.0 na ndizi za kupika kwa asilimia 2.7.
Bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja na mafuta ya taa kwa asilimia 2.9, mkaa kwa asilimia 2.5, dizeli kwa asilimia 4.6, petroli kwa asilimia 2.5 na vifaa vya michezo kwa asilimia 7.8.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Mei, 2016 unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umebaki kuwa asilimia 0.5 kama ilivyokuwa mwezi Aprili, 2016. Aidha, Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 103.00 mwezi Mei, 2016 kutoka 102.46 mwezi Aprili, 2016.
Aidha, ulinganifu wa Mfumuko wa Bei kwa baadhi ya nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki, taarifa hiyo inaonyesha kuwa Mfumuko wa Bei nchini Uganda kwa mwezi Mei, 2016 umeongezeka hadi kufikia asilimia 5.4 kutoka asilimia 5.1 kwa mwezi Aprili, 2016.
Kwa upande wa Kenya, Mfumuko wa Bei umepungua hadi kufikia asilimia 5.00 kwa mwezi Mei, 2016 kutoka asilimia 5.27 iliyorekodiwa mwezi Aprili, 2016.
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa kipimo cha mwaka unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.
MWISHO.
Post a Comment