RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli ameliagiza jeshi la Polisi kutumia mbinu za kisasa katika kukabiliana na uhalifu na kuifanya nchi kuwa sehemu salama nyakati zote.
Dk Magufuli ameonesha kushangazwa na askari wa Jeshi la Polisi kunyang’anywa silaha yake na majambazi na wakati mwingine kuuliwa na majambazi, akihoji uwezo wa majambazi kiasi cha kuwatesa polisi kiasi hicho.
Rais alikuwa akizindua Mpango wa kuboresha usalama wa jamii na mali zao, ambao una dhamira ya kupunguza uhalifu ambapo ameliagiza jeshi hilo kuwahi kushughulikia majambazi kabla ya wenyewe kushughulikiwa na majambazi hayo.
Amesema kama ni silaha polisi wanazo, mafunzo wanayo lakini wanazidiwa na majambazi hadi kunyang’anywa silaha kwanini? Pia Rais amelitaka jeshi hilo kuwashughulikia baadhi ya askari wake ambao hawana nia njema na jeshi hilo.
Awali Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu alisema mpango huo unalenga katika maeneo manne akiyataja kuwa ni Kuboresha mbinuza kupambana na wahalifu na majambazi kwa kuwa na vituo vya polisi vya kuhamahama na kutumia mfumo wa kisasa wa GPS katika doria za jeshi hilo.
Pili, Mangu alisema ni kuongeza ubora wa huduma katika vituo vya polisi ambapo polisi watakuwa wanatatua na kusikiliza kero za wananchi kwa haraka zaidi na kwa muda mfupi sana.
Tatu ni kuboresha mawasiliano ndani ya jeshi la polisi pamoja na jamii. Katika hili IGP Mangu anasema watasaidiwa na mfumo wa GPS katika kuwajua wananchi wanaosumbua jeshi la Plosi kwa kupiga simu za uongo na zenye lengo ovu.
Post a Comment