Stori: Erick Evarist, Risasi Jumamosi
DAR ES SALAAM: Uchumba wa staa wa wimbo wa Chura, Snura Mushi na mwanaume aliyetajwa kwa jina la Ally umevunjika kabla hata wazazi wa msanii huyo hawajatoa majibu ya barua ya posa.
Kwa mujibu wa chanzo makini, kuvunjika huko kunatokana na muoaji huyo kumweleza wazi Snura kuwa, katika maisha yao ya ndoa, yeye hatahusika na matunzo ya watoto wawili ambao staa huyo wa muziki amezaa na wanaume wengine.
“Ndiyo kwanza huyo Ally alikuwa amepeleka posa nyumbani kwa wazazi wake Snura, Mwananyamala (Dar) na ilishapokelewa, alikuwa akisubiri jibu ili kama wakikubali aoe, lakini kwenye uchumba wao ndiyo akamwambia mwenzake hivyo, naye akaona hawezi kukaa na mwanaume ambaye hawataki watoto wake,” kilidai chanzo hicho.
“Kumbe hamjainyaka hii habari? Iko hivi kuna jamaa anaitwa Ally ndiye alimchumbia Snura. Alimtuma mshenga wake anaitwa HK (meneja wa Snura) kwenda kumuwakilisha katika suala zima la kutoa posa,” kilidai chanzo hicho huku kikiomba hifadhi ya jina.
Chanzo hicho kikasema: “Lakini sasa uchumba umevunjika na hakuna ishu tena. Hii ni kama mkosi kwa Snura japokuwa hata mwenyewe Snura alikuwa radhi kwa sababu alizosema jamaa.”
Baada ya kunasa ubuyu huo, Risasi Jumamosi lilimvutia waya HK ambapo alipopatikana alikiri kwenda kutoa posa na kuongeza kwamba, uchumba huo ulivunjika muda mfupi baada ya jamaa kuweka wazi kwamba, anamtaka Snura tu na si watoto wake.
Mama Snura
“Si unajua misimamo, jamaa alitaka kuwa na Snura na si watoto, Snura akaona hawezi kuwatupa watoto wake, anataka kuwalea mwenyewe, na yeye akasema uchumba ufe tu,” alisema HK.
Alipoulizwa Snura kuhusu tukio hilo, alisema alipokea kwa mikono miwili uchumba huo lakini alishangaa msimamo wa mtarajiwa wake huyo wa kutotaka watoto.
“Kuolewa ni jambo la kheri lakini watoto pia ni baraka. Sasa kama mwenzako hataki watoto wako nini kitaendelea? Hata mimi sikuwa radhi, uchumba ukafa,” alisema Snura.
Kabla ya kuchumbiwa na Ally, Snura alishazaa na wanaume wawili tofauti ambao wote safari yao iliishia njiani baada ya kumwagana kwa kushindwana tabia.
Post a Comment