TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa kupokea taarifa za vitendo vya mauaji ya kikatili vinavyoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali nchini, hususani kanda ya Ziwa, Mkoa wa Pwani, na Dar es Salaam.
Wimbi hili la matukio ya vitendo vya mauaji na ukatili uliojitokeza kwa kufuatana mwezi Mei 2016 yanavunja haki ya kuishi ambayo ndio msingi wa haki zote za binadamu kwa ujumla wake.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inalaani vikali mauaji haya yote na matendo yote ya kikatili dhidi ya mwanadamu yanapotokea popote nchini.
Baadhi ya matukio hayo kwa mujibu wa taarifa zilizoifikia Tume yametokea usiku wa Mei 11, 2016 katika kitongoji cha Nyigumba, Kijiji cha Sima Wilayani Sengerema, Mwanza, ambako watu watano (5) wa familia moja waliuwawa kwa kukatwa mapanga; Mei 18 watu watatu (3) pia waliuwawa kwa kukatwa mapanga wakiwa katika nyumba ya ibada, Msikiti wa Rahman, eneo la Ibanda relini, mtaa wa Utemini, Kata ya Mkolani,Wilaya ya Nyamagana, Mwanza; Usiku wa Mei 25, mwanamume mmoja na mkewe waliuwawa kwa kukatwa mapanga kijijini Manzavi, Wilayani Butiama, Mara.
Aidha, mnamo Mei 22, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bulale, Kata ya Buhongwa, Mwanza, Bwana Alphonce Musanyenzi aliuawa. Mauaji mengine yametokea Mei 18, Mkoani Pwani, Askari Polisi, Sajenti Ally Salum Kinyogoli alipouwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika. Mei 23, jijini Dar es Salaam, eneo la Kiwalani, watu wanne (4) waliuawa kwa kuchomwa moto wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao; Mei 26, Bi. Anathe Msuya aliuawa kwa kuchinjwa akiwa nyumbani kwake Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Matukio haya ya ukatili yanakiuka haki ya kuishi iliyoainishwa katika ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria za nchi, matamko na mikataba mbalimbali ya haki za binadamu ya kikanda na kimataifa.
Kufuatia wimbi hili la mauaji linaloonekana kuendelea nchini, Tume inalaani na kukemea vikali vitendo hivyo vya kikatili.
Mbali ya ukiukaji mkubwa wa haki ya msingi ya kuishi, mauaji haya na matukio haya pia ni kinyume na mafundisho ya imani zetu mbalimbali, hivyo yasifumbiwe macho na kuachwa yaendelee, kwani yanaweza kuleta mazoea mabaya ya kuona suala la kuuwa ni jambo la kawaida na hivyo kuhatarisha amani, maisha ya watu na jamii.
Hivyo, Tume inashauri yafuatayo:
1. Serikali kupitia Jeshi la Polisi ichukue hatua mahsusi kuhakikisha ulinzi wa wananchi dhidi ya mauaji na vitendo hivi, kwani jukumu la kwanza la kuhakikisha usalama wa wananchi ni jukumu la serikali. Jeshi la Polisi lihakikishe watu wote waliohusika kutekeleza mauaji haya wanakamatwa ili sheria ichukue mkondo wake.
2. Tume inawataka pia wananchi wahakikishe wanashirikiana na vyombo vya dola kufichua maovu na kubaini uvunjifu wowote wa sheria na haki za binadamu ndani ya jamii, na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuzuia matukio kama haya kujirudia, au kusaidia upelelezi wa mauaji haya na matendo mengineyo ya uvunjifu wa sheria.
3. Jamii ijenge utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu.
4. Mamlaka za Serikali za mitaa katika ngazi zote ziwe na mipango madhubuti ya kuhakikisha ulinzi na usalama katika maeneo yao.
5. Tume inatoa rambirambi kwa ndugu, jamaa na wanafamilia waliopoteza wapendwa wao katika matukio haya na pole kwa majeruhi.
Jukumu la ulinzi na utetezi wa haki za binadamu ni letu sote!
Imetolewa na:
(SIGNED)
Mhe. Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Mei 31, 2016.
Post a Comment