SERIKALI imebaini ufisadi mkubwa ndani ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kutokana na kukamilika kwa kazi ya Tume iliyoundwa mahususi ili kuchunguza utendaji wa mamlaka hiyo, na imeagiza kuchukuliwa hatua kwa watu wote wanaotajwa kuhujumu Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema hayo wakati akizindua Bodi mpya ya TPA inayoongozwa na Profesa Ignas Rubaratuka jijini Dar es Salaam jana.
Akiagiza hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa wahusika waliotajwa katika ufisadi na ripoti hiyo, alisema kwanza ni baadhi kufikishwa mbele ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wengine kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi lakini akionya kuwa ni marufuku kwa wahusika kupewa barua za onyo.
Katika kudhihirisha kukerwa na utendaji wa TPA, Profesa Mbarawa ambaye baadaye alifanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Bandari ya Dar es Salaam, aligoma kukabidhi mabegi ya kuwekea nyaraka kwa wajumbe wa Bodi mpya kwa kusema kuwa yalikuwa ni ya gharama sawa na yale yanayotumika kusafiria Ulaya.
Akizungumzia kukamilika kwa kazi ya Tume, Profesa Mbarawa alisema tume hiyo iliyowajumuisha wataalamu mbalimbali imefanya kazi kubwa ya kuchunguza utendaji wa TPA na kubaini ufisadi mkubwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya mifumo ya miundombinu kama katika mita za kupima mafuta (flow meters).
Kuhusu mita za kupimia mafuta, aliitaka bodi hiyo kuwa makini katika kusimamia utendaji kazi wa mita hizo alizosema serikali imetumia Sh bilioni 12 kuzinunua ili kuhakikisha kuwa zinafanya kazi vizuri na kwamba zinapoharibika ni lazima uamuzi wa ama kununua mpya au kuzirekebisha ufanywe haraka.
Alisema ufisadi mwingine umebainika katika miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ambako mingi imewekwa ili kuwanufaisha watu na si serikali, mgongano mkubwa wa maslahi kwa Bodi ya Zabuni uliochangia kukwama kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo, ajira za kindugu, kulindana, mtandao wa wezi, rushwa na uwezo mdogo wa kiutendaji.
Kuhusu mgongano wa maslahi kwa Bodi ya Zabuni ya TPA, ambayo aliagiza ivunjwe mara moja na kuundwa mpya, Waziri Profesa Mbarawa alisema Bodi hiyo imekuwa ikitanguliza mbele kile alichokiita ‘ten percent’ katika kila zabuni na kukiri wazi kuwa bodi hiyo ni chanzo cha matatizo mengi ya Mamlaka ya Bandari.
Alisema kutokana na udhaifu wa Bodi hiyo ya Zabuni, huduma karibu zote zinazotolewa ndani ya TPA zinatolewa na kampuni ambazo ama ni za wafanyakazi wa mamlaka hiyo, au za waume au wake zao, na kama si hivyo basi ni za ndugu, jamaa au marafiki wa wafanyakazi, jambo linalozua mgongano mkubwa wa kimaslahi.
Kuhusu ajira, alisema ripoti imebaini viongozi wa TPA wamekuwa wakiwaingiza kazini ndugu, jamaa na marafiki zao kinyume cha taratibu za utumishi serikalini na alikwenda mbali kwa kusema kuwa TPA ilipohojiwa kuhusu kasoro hizo kupitia kwa mwanasheria wake ilisema; “hakuna tatizo,” jibu alilosema lilimpa mshituko mkubwa.
Kuhusu mazingira ya rushwa, alimuonya Mwenyekiti wa Bodi hiyo mpya kuwa macho na rushwa, akisema watu wanaohujumu utendaji wa Mamlaka ya Bandari ni watu wanaotumia ushawishi wa kiwango cha juu cha rushwa na kutoa siri kwamba wamewahi kufanya jaribio la kumhonga mjini Mwanza na Dodoma bila mafanikio.
“Ripoti imebainisha kuwa wamekuwa wakihonga hata bodi, wanawapa fedha shilingi milioni tano kwa wajumbe wa bodi na hivyo wanapoteza nguvu ya kusimamia mambo. Ikitokea hivyo kwa bodi hii, wewe ni Profesa mwenzangu kwa hiyo ngoma droo lakini nitakuwajibisha. Nitamwomba Rais akuondoe mlango ulioingilia ndio utatokea na hawa wajumbe ambao wapo katika mamlaka yangu nitawafukuza papo hapo,” alionya Mbarawa.
Post a Comment