Loading...
WANASIASA WAASWA KUACHA SIASA NA MAIGIZO
JUKWAA HURU LA WAZALENDO TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
VIONGOZI WAACHE SIASA, WANANCHI WANATAKA MAENDELEO
Ndugu Waandishi wa habari salaam!
Poleni na majukumu ya kila siku ya ujenzi wa Taifa.
Leo Jukwaa Huru la Wazalendo Tanzania, tumewaiteni hapa kutoa dukuduku zetu kwa mara nyingine tena, juu ya kile kinachoendelea kwa baadhi ya wanasiasa hapa nchini kutaka kuigeuza nchi hii kuwa jukwaa na uwanja wa siasa badala ya kuhamasisha wananchi kujielekeza kwenye shughuli za maendeleo ili kuendana na kasi na azma ya serikali ya kuifanya iwe ya uchumi wa kati mapema zaidi kama dira ya Taifa ya maendelo inavyokusudia.
Tunaeleza masikitiko yetu, hasa kwa upande Kiongozi wa ACT, ndugu Zitto Kabwe, ambaye kwa sasa ameamua kufanya porojo za kisiasa ili kutimiza malengo yake ya kujijenga kisiasa kwa njia ya kukwamisha juhudi na mageuzi makubwa aliyoanza kuyaleta Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Ndugu Zitto anaonekana dhahiri kuwakumbatia na kuwatetea mafisadi na watu walionufaika na unyonyaji wa nchi kwa gharama za wanyonge na wavuja jasho masikini wa Taifa hili. Lakini pia, Watanzania tunajua kiongozi huyu wa ACT, Ndugu Zitto Kabwe si mgeni machoni mwa wananchi kwa siasa zake za maslahi yenye lengo la kujijenga binafsi.
Tunapenda kuuarifu umma kwamba wanasiasa hawa, kwa matendo, kauli na mitandao yao ya kifisadi, hawana mamlaka ya kimaadili ya kumzuia Rais Magufuli kuwatumikia wananchi.
Tunafahamu kwamba juhudi za Rais Magufuli na Serikali yake zimewafanya baadhi ya wanasiasa hawa na mitandao yao kuyumba kiuchumi kutokana na mirija yao kuzibwa, na pia tunafahamu kwamba baadhi wanatumika kukwamisha mageuzi hayo kujaribu kutafuta nusura.
Ndugu waandishi wa habari, hata ukiziangalia na kuzichambua hoja za wanasiasa wetu hawa kumsakama Rais, utaona zina mapungufu makubwa na ni za kushikiwa akili na watu walioko nyuma yao. Hapa tunazichambua kwa kifupi kama ifuatavyo:-
1.Hoja ya mjadala wa Bajeti unaoendelea Bungeni, ndugu Zitto amesimamishwa kwa utovu wake mwenyewe wa nidhamu kwa kukeuka kanuni na maadili ya Bunge.
Sasa unapoharibu mwenyewe Bungeni halafu unakimbilia mitaani kujifanya mchambuzi wa Bajeti ni kusigina misingi ya uwakilishi kwani sisi wananchi tumewatuma wabunge wetu Dodoma sio waje mitaani kutulaghai. Bajeti husoma bungeni na ni bungeni pekee ambapo wananchi huweza kuchangia mawazo ya kuboresha bajeti ya serikali kwa manufaa ya nchi kupitia wawakilishi wao, yaani wabunge. Ndugu Zitto amewanyima fursa wananchi wa Kigoma Mjini ya kuboresha bajeti ya serikali ya mwaka 2016/17 kwa utovu wake wa nidhamu na anastahili kuwaomba radhi.
2.Pia tunapenda umma ufahamu kwamba Ndugu Zitto hawezi kuaminika kama mchambuzi makini wa Bajeti kwa sababu tayari juzi tu aliwadanganya wananchi kwa kueleza uongo kuhusu tozo ya simu na ATM na hajaomba radhi mpaka sasa kutokana na uongo wake huo.
Jukwaa tunamtaka zitto aombe radhi wananchi kwa uongo wa juzi na hivyo anapozuiwa na Polisi asikurupuke kumhusisha Rais lakini pia ajilaumu yeye mwenye kutokana na uongo wake wa kuleta siasa katika masuala ya kitaalamu.
Pia umma ufahamu kuwa katika hili Tanzania inaongozwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni. Bunge ndio eneo rasmi la kutunga sheria, sambamba na upitishaji wa matumizi ya serikali(bajeti) kwa manufaa ya wananchi.
Wabunge kama wawakilishi wa wananchi, jukumu lao mojawapo kubwa ambalo hawawezi kulikwepa, ni kuijadili na kupitisha bajeti ya serikali bungeni ili kuwakilisha mahitaji na vipaumbele vya wananchi kwa faida ya nchi na si kuja kupiga porojo za kisiasa mitaani.
3. Jukwaa limeshangazwa na kusikitishwa na hoja ya eti kuwa Rais ni dikteta, na tunaiona ikirudiwa tena na tena kimkakati ili kujaribu kuzuia mageuzi makubwa anayoyafanya.
Tunawaomba Watanzania waipuuze na kuipuuza hoja hii kwani kama Rais angekuwa dikteta ndugu Zitto mwenyewe asingefanya mkutano Zakheem, Mbagala, wiki iliyopita na asingepata hata hiyo fursa ya kufanya hata mkutano wake na wandishi wa habari na wala asingepata nafasi ya kufanya maigizo anayoyafanya sasa.
Hoja yetu hapa ni kwamba nchi yetu hii adhimu isipakwe matope kwa maslahi ya wachache. Anayedhani Tanzania kuna udikteta atafute nchi moja yenye udikteta akakae japo siku moja kisha atarudi akijutia kauli yake.
Kutokana na kasi ya serikali ya awamu ya tano, wanasiasa hawa wameyumba sana kifikra na kukosa hoja barabara ya kuishika na kubaki kutapatapa; leo utasikia Rais ni dekteta, kesho watamuomba awasaidie maendeleo katika majimbo yao.
Tunawakumbusha wananchi wenzetu kwamba hakuna wakati tunaopaswa kuwa wamoja kama sasa.
Tunahitaji Taifa lenye mshikamano na umoja huku tukitimiza wajibu na ndoto za kuitoa nchi yetu hapa ilipo na kuelekea kwenye ustawi bora zaidi, kiuchumi, kielimu, kiafya, kimawasiliano na maeneo mengine muhimu.
Tukumbuke waasisi wa taifa hili pamoja na kufanya makubwa katika kuutafuta Uhuru, walikuwa na ndoto ya kuiona Tanzania yenye neema zaidi kwa kila mmoja. Wameondoka katika dunia hii ndoto hii ikiwa bado haijatimia ipasavyo.
Leo, Rais Magufuli amekuja kudumisha misingi hiyo kwa kujenga Tanzania bora na yenye kufuata maadili,utii wa sheria,taratibu,miiko na usawa. Tunasikitika kuona wachache wanataka kututoa katika mstari na njia hii yenye neema kwa Watanzania.
Sisi tunasema bayana; Watanzania wawakatae wanasiasa hawa kwa sababu ni sisi watu wa kawaida, ambao tumejionea wenyewe jinsi mafisadi walivyoyafanya maisha yetu kuwa magumu katika miaka ya nyuma.
Tunawaomba wananchi wenzetu tuwakatae mawakala hawa wa ufisadi na tumuunge mkono Rais Magufuli na Taasisi za dola waendelee kuwatumikia wananchi kwa uzalendo na weledi mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.
Imetolewa Dar es Salaam :Tar 14/6/2016
0755178927
Mtela Mwampamba
Katibu wa Jukwaa Huru la Wazalendo Tanzania
Post a Comment