ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe,ameshangaa kutoshtakiwa kwa aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya awamu ya nne, Mustapha Mkulo pamoja na Waziri wa Uchukuzi Omary Nundu kwa sababu walishiriki makubaliano ya ujenzi wa gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mgawe aliyasema hayo jana wakati akitoa ushahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha katika kesi inayomkabili, Mgawe alidai kuwa katika kipindi hicho, hakuvunja Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa vile alisaini mkataba wa makubaliano ya biashara na Kampuni ya China Communication Construction Company Limited (CCCCL) kutokana na masharti ya mkopo kutoka Benki ya Exim ya China.
Mgawe na aliyekuwa Naibu wake, Hamad Koshuma, wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka, kwa kutoa zabuni kwa kampuni ya CCCCL kwa ajili ya ujenzi wa Gati 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Huku akiongozwa na wakili wake, Frank Mwalongo, Mgawe alieleza kwamba TPA ilitangaza zabuni ya kutafuta kampuni ambayo ingefanya kazi ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa gati hizo na katika mchakato wa awali Kampuni ya CPCS ya Canada ilishinda zabuni hiyo.
Alidai kampuni hiyo baada ya kufanya upembuzi yakinifu ilibaini kwamba ujenzi wa gati hizo ungegharimu Dola za Marekani milioni 321 (sawa na Sh bilioni 67.2) na kupendekeza ujenzi huo uwe wa ubia na kwamba TPA inatakiwa kugharamia uchimbaji wa gati hizo.
Alidai baada ya ripoti hiyo ya upembuzi yakinifu kutolewa,TPA haikuwa na fedha za ujenzi na ndipo ikaanza kutafuta fedha katika benki mbalimbali na kupatikana Kampuni ya CCCCL ambayo ilisema ingewezesha kufanikisha upatikanaji wa Mkopo huo.
Alieleza kwamba katika upembuzi yakinifu uliofanywa na Kampuni ya CCCCL ilibainika kwamba gati hizo mbili zingejengwa kwa gharama ya dola za Marekani milioni 500 (sawa na Sh billion 10.2) na kwamba mkopo huo ungepatikana katika Benki ya Exim ya China.
“Ripoti hiyo pia ilieleza kwamba lazima mkopo huo upate dhamana ya serikali na serikali kupitia Hazina walitueleza kwamba wapo tayari kutudhamini na Septemba 2011 Wizara ya Uchukuzi ilituruhusu tufuatilie mkopo katika Benki hiyo,” alidai Mgawe.
Alidai mwishoni mwa Novemba 2011 wakiwa na aliyekua Waziri wa Uchukuzi, walikwenda China kwa ajili ya kuonana na uongozi wa Benki ya Exim kufuatilia mkopo huo ambako walikutana na Makamu Mwenyekiti wa benki hiyo ambaye aliwahakikishia mkopo wa Dola za Marekani 500 kwa ajili ya ujenzi wa gati hizo.
Alidai walipofika nchini humo, walitakiwa kuandika barua rasmi ya kuomba mkopo huo ambao ungedhaminiwa na serikali, ndipo ilipofika mwaka 2012 aliyekua Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo aliandika barua hiyo na kuambatanisha na barua ya makubaliano ya kibiashara kati ya TPA na kampuni ya CCCCL.
Alidai baada ya kuandikwa kwa barua hiyo, alisaini makubaliano ya kibiashara na CCCCL kutokana na matakwa ya Benki ya Exim kwa sababu ndiyo kampuni iliyofanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa gati hizo mbili na mkataba huo unatambua mkopo kati ya benki ya Exim ya China na Serikali ya Tanzania,” alidai Mgawe.
Alifafanua zaidi, Mgawe aliieleza mahakama hiyo kuwa katika kipindi hicho, TPA ilikuwa haina fedha za ujenzi, hivyo walilazimika kutafuta mkopo kuhakikisha kazi hiyo inafanyika.
Aliiomba mahakama hiyo kumwachia huru kwa madai kuwa, hajavunja sheria ya manunuzi na kwamba mchakato huo ulihusisha viongozi mbalimbali wa serikali wakiwamo mawaziri hao.
Loading...
Post a Comment