MKURUGENZI Mtendaji wa makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL Group), Mohammed Dewji, ameungana na matajiri wakubwa duniani, kutangaza azma ya kugawa nusu ya mali zake kusaidia jamii.
Taarifa kutoka mtandao mashuhuri duniani wa Forbes, imesema kuwa Dewji, ambaye ni bilionea kijana kuliko wote barani Afrika, ameingia katika kundi la matajiri hao ambao wametoa ahadi ya kutoa nusu ya mali zao, kusaidia jamii.
“Baada ya kushuhudia umasikini mkali wakati nikilelewa, siku zote nimekuwa nikijisikia kuwajibika kutoa kwa ajili ya jamii yangu,” amesema Dewji katika barua yake ya kutangaza ahadi hiyo, ambayo ameiweka wazi kwa waandishi wa habari.
Alishukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono na kumjengea moyo wa kusaidia jamii na kipekee katika wajibu wake kwa dini yake ya Uislamu wa kutoa na kujali wahitaji na jamii.
Bilionea huyo anakuwa Mtanzania wa kwanza kuungana na matajiri duniani, Bill Gates na Warren Buffett katika kutangaza nia hiyo tangu 2010 na kushauri watu wengine wenye uwezo kujitolea kwa ajili ya jamii.
Kundi la matajiri waliokwisha kutangaza nia hiyo ya kutoa sehemu ya mali zao kwa jamii, limeshafikia 155 kutoka nchi 17, ambapo Juni mwaka huu, kundi hilo linalotambuliwa kwa jina The Giving Pledge, lilitangaza kupata wajumbe wapya 17.
Wajumbe wa mwanzo wa kundi hilo ni pamoja na Eli Broad na mkewe Edythe, John Doerr na mkewe Ann pamoja na mmoja wa wamiliki wa Facebook, Mark Zuckerberg na mkewe, Priscilla Chan.
Mtandao mashuhuri wa Forbes, umemkadiria Dewji kuwa anamiliki mali zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.1, akiongoza kundi la makampuni ya METL nchini Tanzania, linalojihusisha na biashara za viwanda vya nguo, vinu vya unga na viwanda vya mafuta ya kula, huku kinywaji chake cha Mo Cola, kikiuzwa bei rahisi kuliko kununua Coca-Cola.
Loading...
Post a Comment