KAMPUNI ya Reli nchini (TRL) imeanzisha huduma nyingine ya usafiri wa treni kwa Jiji la Dar es Salaam, ambako sasa kutakuwa na treni ya pili itakayotoka kituo kikuu cha reli kwenda Pugu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Masanja Kadogosa, alisema huduma hiyo itaanza kutolewa Agosti mosi mwaka huu.
Kutokana na hatua hiyo, Mkurugenzi huyo alisema anatangaza kubadilishwa muda wa kuondoka treni ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda bara kuanzia Agosti 2 ambapo treni itaondoka saa 9 alasiri badala ya saa 11 kama ilivyozoeleka.
“Kutokana na mabadiliko hayo abiria wanatakiwa kufika kituoni mapema saa 7 mchana na mabadiliko hayo yanahusu treni za abiria ya kawaida zinazoondoka siku za Jumanne na Ijumaa, lakini huduma za treni ya Delux itaondoka muda wake wa kawaida kila Jumapili kwenda Kigoma saa 2 asubuhi,” alisema.
Kuhusu huduma ya pili ya treni kwenda Pugu alisema itakuwa na vituo 10 ambavyo ni Pugu Stesheni, Mwisho wa lami, Gongo la Mbato, FFU Mombasa, Banana na Karakata, vingine ni pamoja na Vingunguti Mbuzi, SS Bakhressa, Kamata na kituo kikuu cha reli Dar es Salaam.
“Huduma hiyo itakuwa kwa awamu mbili asubuhi na alasiri ambapo treni ya kwanza itaondoka kituo cha Pugu saa 12 kamili asubuhi na kuwasili kituo cha Dar es Salaam saa 12 na dakika 55 asubuhi na kufanya safari zake tatu zitakazomalizika saa 11 na dakika 20 jioni na safari ya mwisho ya kuja Dar itakuwa saa tatu na dakika 45 usiku,” alisema.
Loading...
Post a Comment