Mwili wa marehemu Mitiaki Paul.
MANYARA: WAKATI vitabu vya dini vikifundisha wanandugu kukaa pamoja kwa upendo, hali hii imekuwa tofauti kwa familia moja ambapo ndugu wawili waishio katika Kijiji cha Ngoisuku wilayani Simanjiro, Manyara, wameingia kwenye ugomvi mzito na mmoja wao kuuawa kwa kuchomwa mkuki ubavuni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP Francis Massawe.
Kwa mujibu wa chanzo, Mitiaki ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa anamdai mdogo wake huyo memory card aliyokuwa amemwazima siku za nyuma, baada ya kumdai kwa muda mrefu bila mafanikio, alilazimika kuchukua redio ya mdaiwa na kutoa memory card iliyokuwemo kwenye redio hiyo kitendo kilichopelekea mdaiwa kupandisha hasira na kuanza kugombana na kaka yake.
Baada ya ugomvi huo mdaiwa alikimbilia ndani kwake ambapo alitoka huku akiwa ameshika mkuki mkononi na kwenda kumchoma kaka yake tumboni na kuanguka chini huku damu zikimvuja na utumbo kutokeza nje.
Baada ya kutenda kitendo hicho aliuchomoa mkuki na kumwacha kaka yake akigaagaa chini na muda mfupi baadaye alifariki dunia.
Mtuhumiwa huyo wa mauaji alikimbilia kwenye kambi za uwindaji wanyama za ESHKESH zilizo pembezoni mwa kijiji hicho lakini baada ya kubanwa na kiu cha maji kutokana na kukimbia umbali mrefu katika jaribio lake la kutaka kutoroka, alijitokeza kwa wanakijiji hicho ambako alikamatwa na kufikishwa ofisi ya kijiji kabla ya kupelekwa kituo cha polisi Simanjiro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP Francis Massawe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na wanamshikilia mtuhumiwa kwa ajili ya mahojiano kabla ya kumfikisha mahakamani.
“Tukio hilo lilitokea Julai 30, mwaka huu majira ya saa moja na nusu usiku ambapo kijana wa kabila la kimasai jina lake Permet Paul mwenye umri wa miaka 22 anadaiwa kumuua kwa kumchoma mkuki kaka yake aitwaye Mitiaki Paul kisa kikiwa ugomvi wa kugombania memory card,
tunamshikilia mshtakiwa na baada ya mahojiano kukamilika atafikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Massawe.
Post a Comment