Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaalika wafanyabiashara wa Cuba na Serikali ya nchi hiyo kuja hapa nchini kuwekeza katika uzalishaji wa sukari na kujenga viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu.
Rais Magufuli ametoa mwaliko huo leo tarehe 30 Agosti, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba hapa nchini Mhe. Jorge Lopez Tormo.
Dkt. Magufuli amemhakikishia Balozi Jorge Lopez Tormo kuwa Serikali yake itatoa ushirikiano wa kutosha endapo mfanyabiashara yeyote wa Cuba au Serikali yenyewe ya Cuba itajitokeza kuwekeza katika uzalishaji wa sukari na utengenezaji wa dawa za binadamu, na kwamba licha ya Tanzania kuwa na mahitaji makubwa ya bidhaa hizo kuna nchi nyingi jirani na Tanzania zitanufaika.
"Mhe. Balozi ukiniletea huyo mwekezaji hata kesho nitamkabidhi shamba la kuzalisha miwa na kujenga kiwanda cha kuzalisha sukari mara moja ili uzalishaji uanze, tunataka kumaliza tatizo la sukari, uzalishaji wa sasa wa sukari hautoshelezi mahitaji yote ya Tanzania na pia majirani zetu wana upungufu wa sukari" Amesema Rais Magufuli na kuongeza kuwa yapo maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo cha miwa likiwemo eneo la Bagamoyo ambako kuna hekta takribani 10,000.
Hali kadhalika Rais Magufuli amesema Serikali ipo tayari kutoa ardhi kwa mwekezaji yeyote kutoka Cuba atakayekuwa tayari kujenga kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu na vifaa tiba hapa nchini.
Kwa upande wake Balozi Jorge Lopez Tormo amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya katika uendeshaji wa Serikali na amemhakikishia kuwa Cuba itaendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na Tanzania, na ameahidi kufanyia kazi yote waliyoyazungumza.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Balozi wa India hapa Nchini Mhe. Sandeep Arya ambapo Balozi huyo ametoa taarifa ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa baada ya ziara ya Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi iliyofanyika Mwezi Julai mwaka huu.
Katika mazungumzo hayo Balozi Sandeep Arya amesema wawekezaji kutoka India wanaendelea na majadiliano na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) juu ya utekelezaji wa mradi wa kusambaza gesi majumbani kwa ajili ya matumizi ya wananchi na pia wanajadiliana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi juu ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya jamii ya kunde ili kulisha soko kubwa la mazao hayo nchini India.
Kuhusu ujenzi wa kiwanda cha magari cha Tata, Balozi Sandeep Arya amesema mchakato unaendelea na kwamba tayari wameoneshwa eneo la kujenga kiwanda hicho lililopo Kibaha Mkoani Pwani na matarajio ni kuwa ujenzi wa kiwanda hicho utakamilika mwaka ujao.
Kwa upande wake Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na uwepo wa miradi hiyo itakayoleta manufaa kwa pande zote mbili yaani Tanzania na India na ametoa wito kwa pande zote kuharakisha majadiliano ili utekelezaji wa miradi hiyo uanze haraka.
Aidha, Rais Magufuli amewakaribisha wawekezaji wa India kuja kujenga hospitali kubwa za matibabu ya binaadamu na kujenga viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu huku akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa watanzania na wananchi wa nchi nyingine jirani na Tanzania wanaolazimika kusafiri hadi nchini India kufuata matibabu.
"Wambie wafanyabiashara wa India walio tayari kujenga hospitali kubwa, waje na mimi nitawapa ardhi ya kujenga hospitali, wasipoteze muda waje sasa" Amesisitiza Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
30 Agosti, 2016
Loading...
Post a Comment