WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania kuimarisha kitengo cha tathmini ili kuweka viwango halali ambavyo havitawagandamiza wafanyabiashara na uwepo uwazi kuhusu viwango stahili vya kodi wanavyotakiwa kulipa.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Jumapili, Agosti 07, 2016) wakati alipozungumza na viongozi wa mikoa ya Mbeya, Katavi, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Iringa na Njombe mara baada ya kuwasili mkoani Mbeya kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya maonyesho ya nane nane kwa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika mkoani Mbeya.
‘‘TRA waendelee kukusanya mapato vizuri ila kuna wakusanya kodi wanaotaka kuharibu mkakati wa Serikali kwa kufanya mambo ya hovyo kwa kuwaongezea viwango vikubwa vya kodi kuliko kodi stahili wanavyotakiwa kulipa na kufanya suala hili liwe kama tatizo au adhabu kwao jambo ambalo si sahihi. Naagiza watendaji wa TRA wanaofanya hivyo wasakwe na wachukuliwe hatua“, alisema.
‘‘Wafanyabiashara mnaoonewa kwa chuki binafsi na watendaji wa TRA toeni taarifa ili muweze kufanya biashara zenu kwa uhakika bila ya wasiwasi lengo ni kuwafanya muweze kulipa kodi sahihi kwa mujibu wa sheria“, alisema.
Ili kufanikisha mpango huo Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuwasikiliza wafanyabiashara ambao wana malalamiko ya kweli ya kutotendewa haki katika kutozwa kodi kwa sababu mchango kupitia kodi ni kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa Taifa.
Katika hatua nyingine ameitaka idara ya Uhamiaji ijikite katika kudhibiti watumishi wasiokuwa waaminifu ambao wamekuwa wakichukua rushwa kutoka kwa wageni wanaotoka nje ya nchi na kuwaingiza nchini bila ya kuwa na vibali maalumu.
‘‘Ni lazima tuhakikishe hakuna uingiaji holela ndani ya nchi na hasa kwa wanaoingia bila vibali maalumu kwani bila ya kudhibiti suala hilo tunaacha mianya ya kuingia watu wasiokuwa na nia njema na Taifa letu. Watu watakaobainika wameingia nchini bila ya vibali wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria,“alisema.
Alisema kitendo cha mipaka kushindwa kudhibitiwa na kuruhusu uingiaji holela wa watu wasiokuwa na vibali chini kunasababisha Serikali kushindwa kuteleza ipasavyo mipango yake ya kuwahudumia wananchi kulingana na idadi halisi.
Mbali na kuiagiza Idara ya Uhamiaji pia Waziri Mkuu alisema wakuu wa mikoa ya mipakani wana jukumu la ziada la kuhakikisha wanadhibiti mipaka yote na kuhakikisha hakuna watu wanaoingia nchini bila ya kuwa na vibali.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka wakuu wa mikoa kote nchini kuendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika maeneo yao na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani na utulivu ili Watanzania waweze kutekeleza shughuli zao za maendeleo kama walivyojipangia.
“Natambua kuwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama katika maeneo yenu, endeleeni kuimarisha hali ya ulinzi na usalama. Nchi hii tunahitaji iwe tulivu na salama na ni wajibu wenu kuhakikisha kwamba lolote linalotokea mnalikabili vilivyo“, alisema.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Makalla alipokuwa akisoma taarifa ya mkoa huo kwa Waziri Mkuu alisema mkoa huo una jumla ya viwanda 1,653 kati yake vikubwa ni tisa, vya kati 19 na vidogo 1,625 na bado wanaendelea kuzisimamia halmashauri kutenga maeneo zaidi kwa ajili ya kuongeza na kupanua viwanda.
Mhe. Makalla alisema katika eneo hilo la viwanda mkoa una kiwanda kimoja cha kusindika nyama cha Tanganyika Pachers kilichopo wilayani Mbeya ambacho hakijawahi kufanya kazi tangu kilipojengwa na kufungwa mitambo mwaka 1975.
Mkuu huyo wa mkoa alisema usimamizi wa kiwanda hicho uko chini ya Masajili wa Hazina na kwamba tayari kuna muwekezaji amepatikana kwa ajili ya kukiendesha hivyo ameiomba Serikali kuharakisha taratibu za mikataba ili kiweze kuanza kufanya kazi.
Post a Comment