VMM/U.80/8/Vol.I/68 1/09/2016
TAARIFA YA UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 1/09/2016KATIKA UKUMBI WA NEC MJINI DODOMA
Ndugu wandishi wa
Habari.
Tumelazimika kukutana nanyi leo kwa sababu kadhaa za Kisiasa ili kuzungumza nanyi muweze kufikisha ujumbe wetu kwa jamii, moja kati ya hayo ni kitendo cha usaliti, na utapeli wa kisiasa kilichofanywa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kujigamba kwamba wangeitisha maandamano yasio na ukomo wameshindwa kujitokeza na kuandamana sasa wameanza kutoa visingizio vya hadaa, ghiliba na uzushi .
Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe jana alikutana na Waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kudai kwamba wamelazimika kuahirisha maandamano yao kwa muda kwa sababu mbili kuu alizozitaja;
Amesema wameombwa na baadhi ya viongozi Wakuu wa madhehebu mbalimbali ya dini mazungumzo waliyofanya kwa nyakati tofauti na viongozi hao wakiwaomba, wakiwasihi na kuwataka wasubiri kwa wiki mbili au tatu ili viongozi hao wa dini wafanye jitihada za kukutana na Rais John Magufuli kwa lengo la kutafuta suluhu ya kudumu kufuatia mgogoro wa kisiasa uliopo na kuiepusha nchini isiingie katika machafuko ya kisiasa
Akasema si viongozi wa dini peke yake bali pia wamekuwa na vikao vya pamoja na viongozi wa taasisi za kisheria kama vile Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Jukwaa la Katiba ambao wote amedai wamekisihi chadema na kukitaka kisitishe kuitisha maandamano kwa muda ili kutoa fursa ya kuweza kufanyika jitihada za kuitisha mijadala, mazungunzo na majadiliano.
Ndugu Waandishi wa habari,
Kimsingi sababu zote hizo mbili alizozitoa Mbowe na Chadema hazina ukweli, zimekosa mashiko na mantiki. Kilichodhihirika katika maelezo yake ni utapeli, usanii na mwendelezo wa tamthilia ya kisiasa inayoendelea kufanywa na viongozi wa chama hicho kwa dhumuni la kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
Tunasema na kuuita huu ni upuuzi na utoto wa kisiasa , uzushi na uzandiki uliovuka mipaka kwa viongozi wa chama hicho huku baadhi yao wakiwemo wale ambao wamewahi kuitumikia Serikali katika nyadhifaa za juu, pia nao wakidiriki kuudanganya ulimwengu kwa kutoa madai Tanzania kuna mgogoro wa kisiasa ambao unaohitaji kupatiwa suluhu au kufanyika mazungumzo na majadiliano.
Kwa upande wetu UVCCM tumeshangazwa na madai yaliyotolewa na Chadema kupitia kinywa cha Mbowe kwamba chama hicho na viongozi wake wamekuwa wakikutana na viongozi wa madhehebu ya dini na Mashirika hiari ya kiraia, kisheria na kuwataka ati wasitishe maandamano yao haramu kwa muda hadi Oktoba Mosi mwaka huu.
Tumekuwa tukijiuliza bila kupata majawabu ya maana pale Mbowe na Chadema wanaposema kuwa wameshauriwa na viongozi wa madhehebu ya dini na taasisi nyingine za kiraia. Je hapo awali chama hicho kilishirikiana na viongozi hao katika kupanga na kuitisha maandamano haya yenye lengo la kumdhihaki Rais na kumwita kiongozi wa Taifa aliyechaguliwa kikatiba na kisheria kwamba ni dikteta?.
Si jambo linaloweza kuingia akilini na mtu alazimike kuyaamini maneno ya Chadema na Mbowe kama kweli viongozi wa madhehebu ya dini na taasisi zilizotajwa, walihusika kwa namna moja au nyingine kushiriki katika mpango wa uitishaji wa maandamano hayo ya vurugu yanashabihiana sasa viongozi hao wahusike tena kuwashauri na kuwataka chadema kusitisha maandamano.
Aidha kwetu UVCCM, wakiwemo wananchi wema, wapenda amani na utulivu, viongozi wa Mashirika hiari ya kiraia na kijamii na viongozi wa madhehebu mbalimbali za dini, hatuwezi kusimama hadharani na kuithibitishia dunia kwamba katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuna jambo linaloitwa mgogoro wa kisiasa ambao unaohitaji yafanyike mazungunzo, majadiliano hadi kufikia mapatano.
UVCCM tunajua na ulimwengu unafahamu, mashirika na jumuiya za kimataifa zinaelewa kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015, wananchi katika kutekelezawajibu wao wa kikatiba, na kwa kupitia njia ya demokrasia ya Uchaguzi, kwa utashi na ridhaa, walimchagua kwa kumpigia kura Rais Dk. John Magufuli kuwa Rais wao. Matokeo ya Uchaguzi huo yalitangazwa na chombo chenye dhamana ya kisheria na Katiba yaani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC.).
Hata hivyo wananchi wote wanafahamu, Mashirika ya Kimataifa na ulimwengu mzima unaelewa kuwa Dk. Magufuli baada ya kuchaguliwa, Serikali yake bila kupoteza wakati imekuwa ikihimiza kwa nguvu zote katika dhana ya kuimarisha uwajibikaji, utendaji wenye ufanisi na tija, kuwepo kwa nidhamu maeneo ya kazi, Serikali yake ikipiga vita ufisadi na ubadhirifu wa Mali za Umma lakini pia Serikali hiyo ikikusanya kodi na kuongeza Mapato ya Taifa.
Kinachofanywa na Viongozi wa Chadema kila mmoja wetu anafahamu, dunia inajua na Chadema wanafahamu, wana nia na kusudio la kuzizuia jitihada za Serikali ya Rais Dk Magufuki isifike malengo ya msingi huku wakitaka kumkwamisha kiutekelezaji na wao wapate muda wa kumsuta kwamba ameshindwa kutekeleza alichowaahidi wananchi katika Uchaguzi Mkuu.
Chadema na Ukuta wao wanachotaka ni kuendekeza siasa za mitaani, maandamano yasiyo na umuhimu, yakithiri malumbano na mabishano yasiyo na maana badala ya kuwahimiza wananchi wafanyabiashara, wafanyakazi, wavuvi na wakulima wafanye kazi kwa bidii, wajitume, wazalishe mali ili kulijenga Taifa letu kiuchumi na kimaendeleo.
Haipendezi na haiwapi heshima mbele ya jamii watu wanaojiita viongozi wa kisiasa wa chadema wakawa na uhodari wa kutunga uongo, wao wenyewe wa kauamini, kuueneza na kuutetea kwa misuli ya unafiki na upotoshaji kinyume na ukweli wa mambo ulivyo.
UVCCM tunawaasa na kuwaonya viongozi wa Chadema waache mara moja tabia ya utoto wa kisiasa na kuwajengea hofu wananchi, kuwafanya muda wote waiishi kwa wasiwasi kwa matamshi ya siasa zao uchwara ambazo zimekosa afya kwao na wala zisizoweza kuwajenge taji la heshima mbele ya macho ya dunia.
UVCCM tunatamka bayana kuwa hakuna mazungumzo, majadiliano wala mijadala itakayojadiliwa kati ya Serikali ya CCM na Chadema, tunaiomba Serikali ya Rais Dk Magufuli iendelee na mikakati yake ya kisera ili kushamirisha maendeleo ya kiuchumi na juhudi za utekelezaji wa kuiletea mabadiliko nchi yetu ili kuwa ya viwanda sanjari na kupambana na maadui umasikini, ujinga na maradhi.
Hatuwezi kukubali kuweka rehani usalama wa amani ya nchi yetu kwa watu wanaotumika na maadui wa nchi yetu nadhani sasa wamewadhihirishia watanzania kuwa wao kama viongozi wa Chadema hapo ndipo ukomo wao wa kufikiri ulipofia na kuishiwa kabisa na hoja zenye mashiko.
UVCCM tulijua, tulielewa na kutambua mapema kwamba Chadema na viongozi wake walikuwa wakifanya maagizo katika siasa, hawana ubavu wala jeuri ya kuandamana kwa madai ya kipuuzi na ambayo si ya msingi kwa mustakabali wa nchi yetu.
Wameshindwa kuandamana Septemba Mosi, hawataweza na wala hawatajaribu kuandamana Oktoba Mosi, hawataweza kwa sababu wanachotaka kukifanya ni matipwi ya kisiasa, kutaka kucheza mchezo wa rede na nage baada ya kushindwa kubuni mkakati wa kufanya siasa ili Chama chao kiaminike na kukubalika.
Tunaelewa jinsi Wabunge wa Chadema walivyochachamaa na kumbana Mwenyekiti wao kwa nguvu ya hoja huku wakipinga na kutaka warudi bungeni kushiriki vikao kwa sababu kwanza wanazidi kutofahamika kwa wapiga kura majimboni mwao lakini pia wanakabaliwa na ukata mkali na hawaoni kwa nini wasishiriki bungeni wakati baadhi ya viongozi wao wa juu ndani ya Chadema wana utajiri usioelezeka na wengine ni wafanyabiashara .
Tunaamini kuwa viongozi wa madhehebu ya dini , Mashirika hiari ya kijamii na ya kisheria wana uwezo wa kumhitaji Rais , kumpata na kukutana naye ana kwa ana kwa mintarafu ya kujadili masuala mengine ya kimaendeleo na si yale yanayohusu siasa kwa sababu wao si sehemu ya siasa na si wanasiasa.
Ndugu Waandishi wa habari
Mwisho UVCCM tunamsihi tena Ndg. Edward Lowasa Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa aache kusema ovyo kwenye vyombo vya habari kujitafutia sifa zisizo na tija na kwa umri wake sasa ni muda wa kucheza na wajukuu zake.Sio kucheza na akili za Watanzania.
Tunamkumbusha kauli yake aliyoitoa wakati tukielekea Uchaguzi Mkuu, endapo atashindwa Uchaguzi atakwenda kuchunga ng’ombe, nadhani sasa ni muda muafaka kwake kutekeleza kwa vitendo azma yake hiyo.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU
on Thursday, September 1, 2016
Post a Comment