WAKATI Rais John Magufuli wa Tanzania akishikilia msimamo kuwa nchi yake haitasaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) na Umoja wa Ulaya (EU) mpaka dosari kadhaa zitakaporekebishwa, baadhi ya wabunge wa EU wamemuunga mkono na kutahadharisha mkataba wa sasa utaua viwanda vya ndani.
Siku kadhaa zilizopita, msimamo wa Tanzania na Burundi ulilazimisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kukubaliana kusogeza mbele makubaliano ya ama zote zisaini mkataba huo au la ili kuruhusu uchambuzi zaidi.
Tayari nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zimekubaliana na mkataba huo wa EPA huku Tanzania na Burundi zikitoa sababu nzito za kiuchumi, zinazolenga kuhakikisha kuwa kabla ya kusaini mkataba huo, ni vyema suala la ulinzi wa viwanda vya ndani likazingatiwa.
Mkataba huo unapaswa kusainiwa na nchi zote ili uanze kutumika katika ukanda mzima.
Chini ya mkataba huo ambao majadiliano yake yalianza tangu mwaka 2007, EU inaahidi kuzipatia bidhaa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki soko kwa kutotozwa kodi zinapopelekwa kwa nchi wanachama wa Ulaya, lakini na yenyewe italeta bidhaa zake katika soko la ukanda bila kutozwa kodi. Hata hivyo, msimamo wa Tanzania umesimama katika ulinzi wa viwanda vya ndani, hasa wakati huu Serikali ikijikita zaidi katika uchumi wa viwanda.
Msimamo huo sasa unaungwa mkono na wabunge wawili wa EU, Marie Arena na Julie Ward, ambao wanashauri Afrika Mashariki isisaini mkataba huo wa ubia kwa namna ulivyo sasa.
Katika mahojiano yao maalumu na mwandishi wa mtandao wa jarida mashuhuri la The New Times, wabunge hao wanasema bayana kuwa uamuzi wa Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki wa kuahirisha kusaini ubia huo hadi mwakani ili watafakari zaidi uko sahihi.
“Tunaamini mkataba huu kwa namna ulivyo sasa hauko sawa. Ulaya inaitumia Kenya ambayo ndiyo yenye maslahi zaidi katika mkataba huu kuwa kama ngao yao. Wakati Kenya ilishaendelea kiviwanda, hali sio kama hivyo kwa Tanzania, Uganda na Burundi ambazo hazitafaidika.
“Iwapo bidhaa za Ulaya zitaruhusiwa kuingia tu katika ukanda wa Afrika Mashariki italeta ushindani usio wa haki na zaidi nchi hizo zitapoteza kodi katika baadhi ya bidhaa na pia baadhi ya viwanda vitashindwa ushindani na kufa,” wanasema wabunge hao.
Wabunge hao wananukuliwa wakisisitiza kuwa kutokana na hali hiyo, wamejitolea kuzisaidia nchi kama Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa kuzishinikiza nchi za Ulaya zipitie upya ubia huo na kuanzisha mfumo mpya wenye manufaa kwa pande zote.
“Tunadhani nchi hizi zinapaswa kusubiri mpaka zote zitakapoingia katika uchumi wa kipato cha kati ndipo zinaweza kuingia mikataba kama hii yenye kuleta ushindani wa kibiashara. Kwa Rwanda na nchi nyingine za EAC sisi tunaona kwa sasa wangeimarisha kwanza soko lao la ndani katika ukanda huo,” wanaongeza wabunge hao.
Wabunge hao wanafafanua kuwa kwa sasa Kenya, ambayo imeshaingia katika uchumi wa kipato cha kati inaweza kufaidika, lakini wanaonya nchi nyingine hazitafaidika na EPA mpaka hapo watakapofikia uchumi wa kati. Walipoulizwa ni kwa nini wakiwa wabunge wa Ulaya, bado wanapingana na mkataba huo utakaoipa faida za kiuchumi jumuiya yao, wabunge hao walijibu:
“Hoja yetu sio kupinga biashara na Afrika Mashariki, tunachotaka ni kuona ubia huu unanufaisha pande zote. Tunazo taarifa nyingi za kitafiti hata kutoka Kituo cha Kimataifa cha Biashara zinazoonesha kuwa mkataba huu utakuwa na hasara kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.”
Wabunge hao wanazidi kufafanua kuwa mikataba mibovu inayoingiwa na Ulaya na Afrika inaathari nyingi ikiwemo kusababisha umasikini Afrika na matokeo yake kuleta athari mbaya kwa Ulaya ikiwemo kuongezeka kwa wahamiaji haramu.
SERIKALI YATOA BILIONI 14.4 MRADI WA ENGARUKA
37 minutes ago
Post a Comment