Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza awamu ya kwanza ya majina ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini watakaopewa mkopo kugharimia masomo yao.
Idadi ya wanafunzi ambao tayari wamepitishwa kupata mkopo ni 7,904, hata hiyo imeelezwa kiwango hicho kitaendelea kubadilika kwa kuwa mchakato unaendelea.
Taarifa iliyotolewa jana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Stella Manyanya ilibainisha kuwa bodi imekamilisha uchambuzi wa majina ya waombaji ambao wana sifa zinazotakiwa na majina ya wanufaika wapya ambayo yameanza kutangazwa kupitia tovuti ya bodi hiyo.
“Kwa kuzingatia mpango mkakati, pia mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka 2016/17, Serikali imetoa vigezo vitakavyozingatiwa katika utoaji mikopo,”alisema Manyanya.
Alitaja vigezo vilivyotumika kuwa ni pamoja na vipaumbele vya kitaifa vinayoendana na mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na mafunzo ambayo yatazalisha wataalamu wanaokidhi mahitaji ya kitaifa katika fani za kipaumbele.
Manyanya alizitaja fani zilizopewa vipaumbele kuwa ni sayansi za tiba na afya, ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo, mafuta na gesi asilia, sayansi asilia na mabadiliko ya tabianchi, sayansi za ardhi, usanifu majengo na miundombinu.
Katika taarifa yake, Manyanya alisema pia mchakato wa kuwapata wenye sifa za kukopa uliangalia uhitaji wa waombaji, hususan wenye mahitaji maalumu kama walemavu na yatima, ufaulu wa waombaji katika maeneo ya vipaumbele na umahiri.
“Kuanzia mwaka huu wa masomo, wanufaika wote wa mikopo (wapya na wanaoendelea na masomo) watakopeshwa kulingana na uwezo wao katika vipengele vyote vya mikopo,”alisema.
“Kuanzia mwaka huu wa masomo, wanufaika wote wa mikopo (wapya na wanaoendelea na masomo) watakopeshwa kulingana na uwezo wao katika vipengele vyote vya mikopo,”alisema.
Akizungumzia mchakato huo, mkurugenzi mtendaji wa bodi hiyo, Abdul Badru alisema unaendelea kufanywa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na timu ya bodi imejigawa katika vikundi ili kuhakikisha mipango inakwenda jinsi inavyotakiwa.
“Timu ipo kazini na inafanya kazi yake kwa umakini. Kwa sasa majina ya waliochaguliwa kutokana na vigezo yamewekwa, lakini ni wahusika wenyewe au walezi na wazazi ndiyo wanaweza kuyaona kupitia namba zao za usajili wa kidato cha nne. Lakini siku chache zijazo tunaweza kuwataja wakaonekana kwa kila anayehitaji kuyaona,” alisema Badru.
Post a Comment