Wakati Mwenyekiti wa CUF aliyefutiwa uanachama, Profesa Ibrahim Lipumba akitangaza masharti kwa Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad ya kuingia kwenye ofisi za chama hicho Buguruni, Dar es Salaam Chadema imetangaza kutoshirikiana naye.
Akizungumza kwenye makao makuu ya Chadema jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliwataka viongozi wa chama chake, kutotoa ushirikiano kwa Profesa Lipumba, badala yake wampuuze na wamwone kuwa msaliti wa harakati za kudai haki.
Wakati akisema hayo, Profesa Lipumba akiwa katika Ofisi Kuu za CUF, alitoa masharti kwa Seif kama anataka kufika ofisini hapo, kuwa lazima akiri kumtambua na kumkubali kuwa Mwenyekiti halali wa chama hicho.
Mbowe katika mkutano wake na waandishi wa habari, alisema Lipumba, Msajili wa Vyama vya Siasa na taasisi ya utafiti ya Twaweza, ni mawakala wa Serikali wa kuzia harakati za kupigania demokrasia nchini.
Alisema harakati za kuzuia wapinzani kupigania haki, hazifanywi moja kwa moja na Serikali, bali na wakala wao ambao wanakuja kwa sampuli mbalimbali.
“Kamati Maalumu ya Kamati Kuu inatambua mgogoro ndani ya CUF, hivyo chama chetu hakimtambui Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF wala Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa.
“Kamati inalaani uamuzi wa Jaji Francis Mutungi wa kuivuruga CUF kwa kujaribu kumrudisha madarakani Lipumba ambaye alijiuzulu katika mazingira yanayoashiria kununuliwa na CCM, kwa lengo la kusaliti Ukawa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana,” alituhumu.
Kuhusu Jaji Mutungi, Mbowe alimtangaza kama adui wa demokrasia na vyama vingi na kudai kuwa pamoja na kuwa Jaji, hana weledi wa kusimamia vyama vya siasa.
Alitumia nafasi hiyo kubainisha kuwa chama hicho hakina sababu hata moja ya kumheshimu mtu kama Jaji Mutungi ambaye alisema anaonekana kutumika na CCM.
“Mtu ambaye tunamwona msomi, ambaye hapewi mamlaka yoyote ya kisheria ya kuamua ndani ya vyama vya siasa, badala ya kusaidia vyama kumaliza migogoro, amekuwa akichangia migogoro.
“Anaona vyama vinaminywa na Serikali anakaa kimya, lakini kila akizungumza anavikandamiza zaidi, huyu mtu ni adui mkubwa sana,” alisema.
Alimhakikishia Jaji Mutungi kuwa mbinu zake za kudhoofisha vyama vya upinzani hazitafanikiwa, kwani hakuwa Msajili wa kwanza, na kwamba matendo hayo hayatafifisha vyama hivyo.
Kuhusu Twaweza, alidai kuwa imekuwa ikilipwa na Serikali itangaze mambo mbalimbali siku moja kabla ya Ukuta kwa kutoa takwimu alizoziita za kipumbavu na kwamba wamekubali kujitwisha uendawazimu.
“Hawa ni mawakala wa Serikali na wanajulikana. Ni Mtanzania mwendawazimu pekee ambaye utamwambia kwamba hali ya nchi, Serikali inakubalika kwa asilimia 96, lazima uwe mwendawazimu na utafiti huo hauwezi kulisaidia Taifa,” alisema.
Wakati Chadema ikitoa kauli hiyo, hali ya kisiasa ndani ya CUF ilizidi kuwa mbaya kutokana na pande mbili zinazosigana kutunishiana misuli.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari waliofika Ofisi Kuu zaCUF jana, Profesa Lipumba alisema alipata taarifa kwamba Maalim Seif angefika ofisini hapo juzi, hivyo alimsubiri ampangie kazi.
Alisema kama Seif angefika, kabla ya kufanya kazi na Mwenyekiti jambo la kwanza ingekuwa ni kumtambua kwa nafasi hiyo ambayo alivuliwa na kikao kisicho halali.
“Ni lazima akija hapa afanye kazi na Mwenyekiti na walinzi wetu wanamfahamu, wasingemfanya chochote kwa kuwa ni kiongozi wao pia,” alisema na kuongeza:
‘’Huwezi kuja ofisi za chama, halafu ukasema humtambui Mwenyekiti, analijua hilo kwamba akija hapa ni lazima afanye hivyo, kwani anajua kikao kilichokaa Zanzibar ni cha ujanjaujanja.’’
Profesa Lipumba alisema ndiye kiongozi wa walinzi wote wa chama, hivyo wana haki ya kumlinda wanavyotaka wao kwa maslahi ya chama.
Alisema Maalim Seif anatakiwa kujiamini na kufika kwenye ofisi hiyo ili afanye kazi na Mwenyekiti wake za kujenga chama na hakuna kikundi kilichokuwa kimeandaliwa kufanya vurugu au kugombana na kiongozi huyo.
“Anaweza akaja lakini hawezi kusema kuwa kuna kikundi, hawa ni walinzi wanaomlinda tangu anagombea nafasi hiyo mwaka 2014, hatuna kikundi ni Blue Guard na anapaswa kuwaheshimu na si kuwaita kikundi,’’ alisema Lipumba.
Alisema hakuwa na taarifa rasmi ya ugeni wa Maalim Seif, bali alisikia kwenye vyombo vya habari, kwamba atakuja na wabunge pamoja na wajumbe kutoka Zanzibar, hivyo alikuwa anasubiri ujio wake kwa kuwa ana ofisi yake.
‘’Maalim Seif ana ofisi hapa, yeye kuja ni jambo la kawaida, ila tangu nimeanza kufanya shughuli za chama sijamwona ofisini, hana haja ya kutangaza anaweza akaja ofisini kwa Mwenyekiti wake, apate miongozo ya kazi,’’ alisema.
Kuhusu ujio wa wabunge na wajumbe wa Baraza Kuu alisema atawajulisha muda wa kukutana, kwa kuwa hajawaita hawapaswi kufika katika ofisi hiyo kama kikundi.
Habari za ndani kutoka ofisi hizo, zilidai kuwa Lipumba alilala ndani ya ofisi hizo usiku wa kuamkia jana pamoja kundi la wafuasi wake waliokuwa wakihofia kwamba upande wa Maalim Seif ungefika usiku kuchukua ofisi yao.
Mmoja wa wafuasi wa Lipumba ambaye alikuwa katika ofisi hizo jana, alidai baadhi ya wafuasi wa kiongozi huyo walikesha hapo kwa lengo la kumlinda kwani alikuwa anafanya kazi zake.
‘’Lipumba hakubaki ofisini kwa kuogopa kundi la Maalim Seif ila alikuwa akifanya kazi zake kwa kuwa ni muda mrefu tangu ajiuzulu hakuwa ofisini hivyo kazi zimezidi,’’ alisema.
Hata hivyo, Lipumba alikana kulala ofisini bali alifika saa 1:45 asubuhi.Katika ofisi hizo magari ya Polisi yalikuwa hayakauki kuanzia saa moja asubuhi huku Lipumba akieleza kwamba hakuomba msaada wala ulinzi wowote wa Polisi, kwa kuwa alikuwa ofisini.
Juu ya taarifa kwamba Maalim Seif aliomba ulinzi Polisi, wamsindikize alisema ni jambo la ajabu.
‘’Ikiwa kuna ukweli katika hilo nastaajabu, unaomba ulinzi kwenda ofisini kwako, ina maana walinzi alionao wa Serikali na wana chama hawatoshi?’’ Alihoji Lipumba.
Post a Comment