WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga na kuhakikisha sekta ya mifuko ya jamii inaboreshwa na kwa kuzingatia hilo imelipa deni la zaidi ya Sh bilioni 722.7 lililokuwa likidaiwa na mifuko hiyo.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema hayo jana katika Mkutano Mkuu wa Sita wa Wadau na Wanachama wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) uliofanyika jijini Arusha, akieleza kuwa deni hilo ni kati ya madeni ya michango ya jumla ya Sh bilioni 964.2.
Alisema serikali inakamilisha uhakiki wa madeni ya miradi ya mifuko ili itoe hati fungani na katika kipindi kinachoishia Juni mwaka huu takwimu zinaonesha idadi ya wanachama imeongezeka hadi kufikia milioni 2.1.
Waziri Mkuu aliwaambia wanachama na wadau kuwa katika kubana matumizi Serikali ya Awamu ya Tano imehakikisha gharama za uendeshaji wa mifuko zinapungua kutoka asilimia 19 ya michango ya wanachama hadi kufikia asilimia 10 kwa mujibu wa kanuni za gharama za mifuko zilizotolewa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).
Alisema serikali imejipanga kuona nchi inapata maendeleo ya haraka kwa manufaa ya Watanzania wote katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imelenga kuiwezesha nchi kuwa ya uchumi wa kati wenye kujengwa na viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu na kupunguza umasikini.
Waziri Mkuu alifarijika kusikia kuwa NSSF imedhamiria kwenda na mwendo huo kwa kupanua wigo wa uwekezaji wake na kuelekeza katika viwanda jambo ambalo litaongeza ajira, kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa jumla.
Alisema maamuzi hayo yataiwezesha NSSF na mifuko mingine kupata wanachama wapya na kukusanya michango zaidi na kuiwekeza ili kutimiza lengo lake la msingi la hifadhi ya jamii.
Alisema uamuzi wa NSSF na PPF kuungana ili kukabiliana na tatizo la sukari nchini kwa kujenga kiwanda cha sukari mkoani Morogoro eneo la Mkulazi kitakachoweza kuzalisha tani 200,000 kwa mwaka na kuajiri watu zaidi ya 100,000 huo ni moyo wa uzalendo ambao unafaa kuigwa na kila mtu na taasisi na kampuni mbalimbali nchini.
Alisema mashirika mengine pia yatafakari kuhusu namna ya kukuza uchumi wa nchi na wananchi wake na si kujikita tu katika malengo machache ambayo hayawafikii wananchi kwa mapana na uwazi zaidi.
Alitoa mwito kwa waajiri nchini kuhakikisha wanawasilisha malipo ya wanachama wao kwa wakati bila ya kusukumwa ili shirika hilo lifanye kazi zake kwa ufanisi mkubwa.
Naye Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alimwambia Waziri Mkuu kuwa agizo lake la kukusanya madeni yote sugu limeanza kutekelezwa kwa amri ya Bodi ya shirika hilo bila ya kipingamizi.
Jenista alisema wadaiwa sugu waliokuwa wakipangisha nyumba hizo na wale walionunua na kushindwa kuwasilisha malipo hatua kali za kisheria zinaandaliwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi.
Alisema uwekezaji wa sasa ni uwekezaji wa viwanda hilo halina ubishi kwa shirika hilo na menejimenti na bodi kwa pamoja wamejipanga kuhakikisha malengo hayo yanatimia.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara amesema kuwa shirika hilo limejizatiti kuwekeza katika sekta ya viwanda nchini sambamba na kuinua viwango vya ajira nchini na kuboresha maisha ya wanachama wa mfuko huo na wananchi kwa ujumla.
Profesa Kahyarara alisema wameamua kufanya mageuzi makubwa katika uwekezaji kwa kulenga uwekezaji utakaowagusa moja kwa moja wananchi na kuyabadili maisha yao kuwa bora, na wameamua kuelekeza ufanisi na kuleta tija kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi na wananchi wake kwa kuongeza ajira na kuongeza wanachama wake.
Hatuna huruma, tunabeba vyote-Dk. Biteko
25 minutes ago
Post a Comment