WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameunga mkono marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa ajili ya kumpa uwezo Rais kuteua wajumbe wa Baraza bila ya kushauriana na kiongozi wa upinzani huku wakitaka marekebisho mengine zaidi kwa lengo la kuleta ufanisi.
Mwakilishi wa Jimbo la Shauri Moyo, Hamza Hassan Juma alisema wakati umefika sasa kwa Katiba ya Zanzibar izingatie demokrasia ya mfumo wa vyama vingi kwa vitendo na kuacha kuweka kipaumbele kwa vyama vya CCM na CUF.
Alisema athari za kuvishirikisha vyama hivyo, ikiwemo katika Katiba imeanza kuonekana ambapo mwaka jana viongozi wa CUF walisusia Baraza la Wawakilishi wakati wa kupitisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Chaani, Nasir Abdulatif Jussa (CCM) alisema marekebisho yatakayopitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi yatampa uwezo mkubwa Rais wa Zanzibar sasa kuchagua wajumbe wa Baraza la Wawakilishi bila ya kupata ushauri kutoka kwa mtu yeyote.
Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Said Hassan Mzee alisema marekebisho hayo ni muhimu ambayo yataondoa masharti na kumpa uwezo Rais kushauriana na kiongozi wa upinzani ambaye kwa sasa hayupo.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipitisha muswada huo wa Marekebisho ya 11 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambayo sasa yatampa nafasi Rais wa Zanzibar kuchagua wajumbe wawili wa Baraza la Wawakilishi katika nafasi 10 bila ya kushauriana na kiongozi wa upinzani ambaye katika muundo wa Baraza la Wawakilishi la sasa hayupo.
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa sasa wajumbe wake wote wanatoka CCM baada ya kushinda majimbo yote ya Unguja na Pemba kufuatia CUF kususa uchaguzi wa marudio.
Loading...
Post a Comment