WAKAZI wawili akiwemo Mustafa Kassimu (75) ambaye ni mganga wa tiba za asili katika wilaya ya Korogwe mkoani Tanga na fundi wa kushona nguo, Rashidi Singano (70) wa wilayani Lushoto, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kubaka na kulawiti wanafunzi 11 wa shule za msingi.
Katika tukio la kwanza la Januari 24, mwaka huu, Polisi inamshikilia fundi cherehani huyo ambaye anaishi Kijiji cha Mshwamba Kata ya Lunguza wilayani Lushoto kwa tuhuma za kubaka na kulawiti kwa nyakati tofauti watoto 10 (majina yamehifadhiwa).
Mtuhumiwa huyo inadaiwa alitumia ushawishi wa kuwapa fedha kati ya Sh 300, Sh 600 hadi Sh 1,000 na kuwavizia njiani, kama mbinu ya kuwanasa watoto hao, ambao wote ni wanafunzi katika moja ya shule ya msingi iliyopo Kata ya Lunguza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba alithibitisha tukio hilo kwa kuwaeleza waandishi wa habari kwamba walipata taarifa za ukatili dhidi ya watoto hao kutoka kwa mwalimu wa watoto hao, ambaye jina lake limehifadhiwa.
“Tulipokea taarifa kuhusu tukio hilo kutoka kwa mwalimu wa shule wanayosoma watoto hao, akidai kwamba siku hiyo akiwa shuleni, aligundua kuwa wanafunzi kumi wa kike kati yao sita wote wakiwa wamebakwa, huku wengine wanne wakiwa wamelawitiwa kwa nyakati tofauti na fundi cherehani huyo,” alieleza.
Aliongeza, “Mwalimu huyo alitaja wanafunzi wengine watano na kudai kwamba hao wamenusurika kunaswa kwenye mtego wa kutendewa ukatili huo na Mzee Singano ambaye anaishi maeneo ya jirani na shule hiyo,” alieleza Kamanda Wakulyamba.
Alisema katika uchunguzi, imebainika kwamba mtuhumiwa alikuwa akifanya vitendo hivyo vya kubaka na kulawiti watoto hao ndani ya nyumba anayoishi pamoja na kufanyia shughuli hizo za ushonaji, na aliwapata wakati walipokuwa wakienda kupeleka nguo na wakati wa mchana wanapotoka shuleni kurejea nyumbani.
“Chanzo cha tukio hili kwa kweli ni tamaa mbaya za kimwili alizokuwa nazo mtuhumiwa ambapo alikuwa akiwalaghai wanafunzi hao kwa kuwapa fedha kati ya shilingi mia tatu hadi mia sita wakati wanapopeleka nguo zao kushonwa,” alifafanua.
Tukio la pili linamhusisha mtoto mwingine mwenye umri wa miaka 12, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu (jina limehifadhiwa) wa Kijiji cha Fune wilayani Korogwe aliyelawitiwa na Kassimu (75) wakati alipokuwa akimpatia matibabu ya asili, yaliyolenga kumwongezea nguvu za kiume.
Rais Samia apongezwa kuwezesha ujenzi ofisi kuu za WMA
36 minutes ago
Post a Comment