Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemsimamisha kazi Kaimu Katibu wa Tume ya Mipango (Wizara ya Fedha), Florence Mwanri aliyeidhinisha kuanza kwa awamu ya pili ya ujenzi wa jengo jipya la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) (Terminal 3) kabla ya kumalizika kwa awamu ya kwanza.
Rais Magufuli alifikia uamuzi huo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa jengo jipya na kuagiza shughuli za ujenzi wa uwanja huo ziendelee kuanzia leo.
Katika ziara aliyoifanya jana ilielezwa kuwa mkandarasi anayejenga uwanja huo, kampuni ya BAM International alitangaza kusitisha ujenzi kuanzia jana kutokana na kutolipwa madai yake. Hata hivyo, Rais Magufuli ameahidi kulipa fedha hizo haraka.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ilieleza kuwa Rais Magufuli alisikitishwa na namna mradi huo unavyotekelezwa, ikiwamo Serikali kukubali gharama kubwa za mradi ambazo ni Sh560 bilioni kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na jengo linalojengwa.
“Hivi kulikuwa na sababu gani za ninyi wataalamu wa Serikali kukubali gharama kubwa namna hii, hivi hili jengo linafanana na Sh560 bilioni?
“Halafu mlikuwa na haraka gani kuidhinisha kuanza awamu ya pili ya ujenzi kabla ya kumaliza awamu ya kwanza?” alihoji Rais Magufuli.
Alimuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuunda timu ya wataalamu watakaofanya tathmini ya utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kuzungumza na mkandarasi anayejenga uwanja huo na mhandisi mshauri ambao wamekubali kupunguza gharama za ujenzi wa mradi huo.
Loading...
Post a Comment