UKIWA umebaki mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti mjini Dodoma, mawaziri 13 wanakabiliwa na mtihani mgumu kutokana na ugumu wa utekelezaji wa bajeti za wizara zao kwa mwaka huu wa fedha.
Mawaziri hao ni Prof. Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi), Ummy Mwalimu (Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto), Prof. Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano) na Mhandisi Gerson Lwenge (Maji na Umwagiliaji).
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene.
Wamo pia wasaidizi wa mawaziri hao ambao ni Mhandisi Stella Manyanya (Elimu), Dk. Hamis Kigwangalla (Afya), Edwin Ngonyani(Ujenzi), Mhandisi Isack Kamelwe (Maji), Selemani Jafo (Tamisemi) na Dk. Ashatu Kijaji (Fedha).
Katika bajeti hiyo ya kwanza kwa serikali ya awamu ya tano (2016/17), Bunge liliidhinisha matumizi ya Sh. trilioni 29.53 kwa mwaka huu wa fedha.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 17.72 ni za matumizi ya kawaida, wakati Sh. trilioni 11.82, sawa na asilimia 40 ya bajeti nzima, ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Kufika kikomo kwa bajeti hiyo ambayo imebakisha siku 123, ni mwanzo wa utekelezaji wa bajeti ya pili chini ya uongozi wa Rais John Magufuli itakayopitishwa na Bunge.
Katika mahojiano na Nipashe mwishoni mwa wiki, mawaziri kivuli wa wizara mbalimbali, walisema utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17 umekuwa wa kusuasua na kuna hatari mipango mingi ya maendeleo isitekelezeke, ingawa mawaziri wana muda wa siku 123 kuanzia leo kuhakikisha wanatekeleza bajeti zao kabla ya mwaka wa bajeti kufikia kikomo Juni 30, mwaka huu.
"Tumeshuhudia kwa muda mrefu wizara zimekuwa zikitatua matokeo ya matatizo badala ya kutatua matatizo yenyewe.
Shida si wizara, bali nchi haina hela," alisema Dk. Godwin Mollel, Waziri kivuli wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambaye ni Mbunge wa Siha (Chadema).
Aliongeza: "Unaposema wizara hazitekelezi miradi, zinatoa wapi fedha? Na kama mfuko mkuu wa serikali hauna fedha, zitatekelezaje miradi? Lazima tutafute namna ya nchi ipate fedha."
Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Suzan Lyimo, alisema kuwa upinzani kwa kushirikiana na kamati za kudumu za Bunge, watahoji kwanini serikali haitoi fedha zilizoidhinishwa na Bunge wakati wa vikao vijavyo vya Bunge la Bajeti.
Mtihani unaowakabili mawaziri hao ni kuhakikisha bajeti za wizara zao zinatekelezwa kabla ya Juni 30 huku uzoefu ukionyesha kamati za kudumu za Bunge zimekuwa zikiishia Machi 31 ya kila mwaka kuchambua utekelezaji wa wizara husika kabla ya kuingia kwenye Bunge la Bajeti.
Kutokana na uzoefu huo, mawaziri wana siku 35 kuhakikisha wanafanya walau mambo machache ambayo yatawasaidia kukwepa kushambuliwa na wabunge kwa kuwasilisha bajeti 'hewa' bungeni.
Miongoni mwa mitihani migumu inayowakabili mawaziri hao ni ajira, nyongeza ya mishahara na malipo ya malimbikizo ya madeni kwa watumishi wa umma, uhaba wa dawa na vifaa tiba, ujenzi wa miundombinu ya maji, ujenzi wa meli Ziwa Victoria na ukarabati wa meli zilizopo kwenye maziwa makuu na utekelezaji wa ugawaji wa Sh. milioni 50 kwa kila kijiji/mtaa.
Wakati wa Bunge lililopita la bajeti, ilibainika kuwa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/16 haukuwa wa kuridhisha.
Katika mapitio ya bajeti hiyo bungeni, ilibainika kuwa karibu wizara zote zilikuwa zimepata chini ya asilimia 40 ya bajeti ya maendeleo iliyokuwa imepangwa huku zingine zikiwa hazijaambulia hata senti moja hadi kufikia Machi 31, 2016.
Kwenye bajeti hiyo, Bunge liliidhinisha Sh. trilioni 22.45. Kati yake, Sh. trilioni 16.7 zikiwa za matumizi ya kawaida ambayo ni sawa na asilimia 74.3 ya bajeti nzima huku Sh. trilioni 5.76 (asilimia 25.7) zikitengwa kwa ajili ya maendeleo.
Bajeti kwa miezi minne (Julai mosi hadi Novemba 4, 2015) ilitekelezwa chini ya uongozi wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kabla ya Rais Magufuli kukabidhiwa nchi Novemba 5, 2015 na kuendelea nayo hadi ilipofika kikomo Juni 30.
Swali linabaki, je, mawaziri hao wataweza kutekeleza bajeti za wizara zao ndani ya siku 123 zilizobaki kabla ya kufikia kikomo kwa mwaka huu wa bajeti?
Usikose kufuatilia mwendelezo wa uchambuzi huu wa Nipashe kesho.
Post a Comment