SIKU chache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwafukuza wanachama wake 12, akiwamo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba, baadhi ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wametoa maoni tofauti kuhusu hatua hiyo, wengine wakitofautiana nayo na wengine kuiunga mkono.
Machi 11 mwaka huu, mbali na chama hicho kuwafutia uanachama viongozi wake hao, pia kilitoa onyo kali kwa wanachana wengine 12 baada ya Halmashauri Kuu kupokea taarifa ya tathimini ya Uchaguzi Mkuu uliopita.
Mbali na timua timua hiyo, juzi pia Mkutano Mkuu wa chama hicho, uliridhia mapendekezo ya mabadiliko ya wajumbe wa sekretarieti yaliyowasilishwa na Mwenyekiti Rais Dk. John Magufuli, ambayo pia yamemwondoa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
Wengine ni Katibu wa Uchumi na Fedha, Zakia Meghji ambaye ameteuliwa kuingia katika kamati ambayo itafanya tathimini ya Uchaguzi Mkuu visiwani Zanzibar na Katibu wa Oganizesheni wa CCM, Muhamed Seif Khatib.
PROFESA MPANGALA
Akitoa maoni yake jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea urais ndani ya CCM, ni makada wengi walijitokeza, lakini kinachoshangaza waliochukuliwa hatua ni wale waliokuwa wakimuunga mkono Edward Lowassa.
Alisema ni haki ya kidemokrasia mwanachama wa CCM kumuunga mkono yule anayeona anafaa, hivyo haikuwa kosa kwa makada hao kumuunga mkono Lowassa katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
“Kinachoonekana waliochukuliwa hatua ni wale waliomuunga mkono Lowassa, sasa ninajiuliza ni kwanini wakawaacha wakati ule? Na waliogombea na kuonyesha upande walikuwa ni wengi mbona hawajaguswa?
“Kwa msingi huu, waliotimuliwa wameonewa… hii si dalili nzuri, inaua demokrasia na si nzuri kwa maendeleo ya chama chenye heshima na chenye uzoefu kama CCM,” alisema Profesa Mpangala.
DK. BANA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema timua timua iliyofanyika ndani ya CCM ni kuwarudisha watu kwenye maadili na kwamba hakuna aliye juu ya chama.
“Kilichofanyika ni kizuri, wale ambao hawana utii lazima wawajibishwe, mfano kina Sophia Simba hawakukubaliana na maamuzi ya Kamati Kuu wakati ule na ilikuwa utovu wa nidhamu… lazima uheshimu maamuzi ya wengi.
“Kwanza ni wanafiki kwa sababu wangekuwa wanampenda kweli Lowassa, wangeonekana siku ile ile nao wangeondoka naye kwenda Chadema,” alisema Dk. Bana.
DEUS KIBAMBA
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema atakuwa kichaa akisema waliotimuliwa wameonewa kwa sababu utaratibu kama huo huwa unafanywa na vyama vyote duniani.
Alisema kinachomshangaza ni CCM kuwatimua makada hao kutokana na kuwa na maoni tofauti kuhusu mgombea ambaye wanamtaka.
“Ingekuwa wamefuja fedha, wameiba mali za chama, wamekichafua chama labda wamelewa, makosa yoyote yanayovuruga chama ningewaunga mkono kwa asilimia 100, lakini kosa lao ni kuwa na maoni tofauti kuhusu mgombea wanayemtaka.
“Imenishangaza sana ingekuwa wamefanya hayo baada ya uteuzi wa chama halafu wakatoka kwenda kumuunga mkono mgombea wa chama kingine, hapo sawa.
“Vyama vya siasa vikiendelea hivi, kwamba wanaokuwa tofauti juu ya wanayempenda, ukiwa na maoni tofauti unafukuzwa, basi hiyo demokrasia itakoma kabisa, kwa sababu hata sasa vyama vyote hakuna demokrasia, hata vya upinzani mtu akitofautiana na mwenyekiti anafukuzwa uanachama,” alisema Kibamba.
Kibamba alisema kilichofanyika Dodoma inaweza kutishia wale waliobaki ndani ya chama, kwamba wataogopa kunyanyua midomo yao kutoa maoni tofauti, jambo ambalo ni hatari.
“Hawa waliofukuzwa uanachama wasifikirie sana kujiunga na vyama vingine, wajiunge kupigania mgombea binafsi, ninawakaribisha waje wajiunge kwenye kampeni ya kupigania mgombea huru,” alisema Kibamba.
MADABIDA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, ambaye ni miongoni mwa waliovuliwa uanachama, alisema kwa ufupi: “Sipo tayari kuzungumzia jambo hilo kwa sasa.”
MSUKUMA
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Geita, Joseph Msukuma, alisema taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa ametoa siku saba kwa Usalama wa Taifa kuomba radhi si za kweli.
Jumamosi iliyopita, Msukuma, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Adam Malima na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, walikamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutaka kufanya uchochezi na vurugu wakati wa vikao vya chama hicho.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Msukuma alisema sauti inayosikika kwenye mitandao ya kijamii si yake.
“Hiyo sauti si yangu na RPC nimemsikia leo (jana) kwenye redio ameshaomba radhi. Kwaheri,” alisema Msukuma kwa ufupi.
Jana, gazeti moja la kila siku lilimnukuu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa akisema kwamba wabunge hao waliokamatwa baada ya kuhojiwa, iligundulika kuwa hawakuwa na kosa lolote.
Mambosasa alisema kulikuwa na tuhuma kwamba makada hao watatu walikuwa wakigawa fedha kwa wanachama ili kuchochea vurugu katika vikao vya CCM.
“Tumefunga jalada lao baada ya kugundua kinachosemwa ni tofauti na kilichopo na tumewarudishia fedha zao,” alinukuliwa.
Loading...
BLOG RAFIKI
-
-
-
-
-
VOA Express2 hours ago
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
Post a Comment