Bunge limeelezwa kuwa, Wizara ya Nishati na Madini inahitaji Sh2 bilioni kwa ajili ya kusambaza gesi majumbani katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alisema jana kuwa, mradi wa usambazaji gesi unaweza kukamilika ifikapo mwezi Julai.
Dk Kalemani alitaja kiasi kamili cha gesi kinachohitajika kwenye nyumba za watu katika mikoa hiyo ni mita za ujazo kati ya milioni tano hadi 10 ambazo uwezekano wa kupatikana ni mkubwa kwa kuwa gesi ipo ya kutosha.
Naibu waziri huyo alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma aliyetaka kujua kiasi na gharama zitakazotumika kwa ajili ya usambazaji majumbani.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua ni lini Serikali itasitisha usafirishaji wa gesi kutoka Mtwara kwenda Kinyerezi Dar es Salaam, ili wananchi wa Mtwara waweze kunufaika kwanza na ajira zitokanazo na uchakataji wa gesi hiyo asilia na kujenga viwanda.
Hata hivyo, naibu waziri alisema sera mpya ya nishati ya mwaka 2015 na Sera ya Gesi ya mwaka 2013 zinalenga kutoa fursa ya gesi asilia kuwanufaisha Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na wananchi wa eneo inakopatikana rasilimali hiyo.
Alisema kuna miradi miwili inayosafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam. Dk Kalemani alisema mradi mmoja ni mpya unaosafirisha gesi kutoka Mtwara ambao ulikamilika mwaka 2015, huku mwingine ni wa Songas uliokamilika mwaka 2004 wakati gesi inayochakatwa Madiba, Mtwara inasafirishwa kwa bomba kwenda Mkuranga.
Alisema Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inatekeleza mradi wa kuunganisha gesi hiyo katika Kiwanda cha Dangote kilichopo Mtwara ambacho kitahitaji takriban futi za ujazo 45 milioni.
Post a Comment