Baadhi ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameibuka na kupinga vikali gharama za matumizi ya Faru Fausta aliyepo katika Hifadhi ya Ngorongoro, na kuongeza kuwa gharama hizo haziendani na uhalisia.
Mjadala huo uliibuka mara baada ya Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema) kuuliza swali kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe kuhusu mipango ya Serikali kwa Faru huyo.
Aidha, akijibu swali hilo, Prof. Maghembe amesema kuwa Faru huyo anatumia gharama kubwa za matunzo kwa sababu ni mzee na huwa anaugua mara kwa mara.
“Hivi sasa utafiti unafanyika kwa kumtumia Faru Fausta juu ya namna ya kuishi na wanyama wa aina hiyo ili waweze kuishi maisha marefu, ni kweli kufanya hivi ni gharama kubwa sana,”amesema Prof. Maghembe.
Gharama za matunzo ya Faru Fausta kwa mwezi ni shilingi milioni 64, kiasi ambacho kiliwashtua baadhi ya wabunge na kutaka muongozo zaidi wa kupata taarifa za kina zaidi.
Hata hivyo, kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Fredy Manongi amesema kuwa Faru Fausta ni Mzee na ana umri wa miaka 54, hivyo alipokuwa porini alikuwa akishambuliwa na Fisi kitendo ambacho kilimsababishia vidonda vingi.
Post a Comment