Vitendo vya wanafunzi kupewa mimba vinazidi kuendelea ambapo Leah Mwakyembe (15), mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ikimba na mkazi wa Kata ya Ikimba wilayani Kyela, Mkoa wa Mbeya, anadaiwa kupewa ujauzito.
Mkuu wa Shule hiyo Zawadi Mpunji, alisema alifuatwa na baba mzazi wa mwanafunzi huyo, Abdalah Mwakyembe, akidai ana hofu kuwa mwanawe ana ujauzito ambapo mikakati ya kupima ilifanyika.
Alisema baada ya kumwita shuleni mwanafunzi huyo ambaye inadaiwa alianza utoro siku nyingi, ikabidi wampeleke hospitali ya Wilaya na kubainika kuwa ana ujauzito wa miezi minne na kuwa ilibidi bodi ya shule waandike barua kuhusu taarifa za mwanafunzi huyo, nakala ikapewa serikali ya kijiji na ofisi ya elimu.
Alisema yeye kama mkuu wa shule amekamilisha taratibu za kishule na kumfukuza rasmi mwanafunzi huyo na kuiachia serikali kuendelea na taratibu nyingine za kisheria.
Baba mzazi wa mtoto huyo, Abdalah Mwakyembe, alisema mwanawe alikuwa mzuri kitaaluma na kuanza kushuka ghafla, huku akiwa mtoro. Ilifika hatua anaficha nguo za shule kwenye mashamba ya migomba na kusingizia hana nguo na alipobaini alitoa ripoti shuleni.
Afisa Mtendaji wa Kata hiyo Stephen John, amethibitisha kuwapo kwa taarifa hiyo na kusema wamekamilisha taratibu zote na kukabidhi ripoti kwa afisa elimu na kwa Jeshi la Polisi wilayani humo kwa hatua za kisheria.
Alisema juhudi za kumpata mwanaume aliyempa ujauzito ili achukuliwe hatua bado hazijazaa matunda, baada ya mwanafunzi huyo kutotoa ushirikiano wa kumtaja ambapo awali alipohojiwa alimtaja mfanyabiashara wa viatu, na baada ya kumfuatilia ilibainika kuwa anadanganya.
CREDIT: MTANZANIA
Loading...
Post a Comment